Habari Mseto

Wauguzi wasema hawana uwezo kukabiliana vilivyo na virusi vya Corona, kaunti nyingi nazo haziko tayari

March 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

MUUNGANO wa Kitaifa wa Wauguzi Nchini (NNAK) umesema hauna uwezo wa kukabiliana na virusi vya Corona iwapo kutagundulika kisa cha maradhi hayo nchini huku ikifichuka kaunti nyingi nazo hazijajiandaa ikitokea hali ya aina hiyo.

Kulingana na Rais wa NNAK Bw Alfred Obengo, japokuwa ni jambo la kawaida kwa wahudumu wa afya kuwa na wakati mgumu wakati wa visa kama hivi, kuna umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa vitengo mbalimbali serikalini.

“Ni jambo la kawaida kuhisi kwamba hatuna uwezo wa kukabiliana na mkurupuko kama huu lakini kuna haja ya mafunzo kwa watakaohudumia wagonjwa iwapo mkurupuko kama huu utatokea nchini,” alisema Bw Obengo.

Bw Obengo alikuwa akizungumza katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ambapo vtanda 11 vimetengwa vya kuwahudumia wagonjwa wa maradhi ya Corona iwapo maambukizi yatagundulika.

Bw Obengo aliitaka serikali kuwapa wauguzi msaada kama kuwaandaa kisaikolojia ili wasiathirike baada ya huduma.

Aliilaumu serikali kwa kutozingatia sheria za kiafya ilipowaambia raia hao kujifanyia karantini wenyewe.

“Karantini inapaswa kufanywa kwa umakini sana na wataalamu wa kiafya ndio wanafaa kuongoza jinsi shughuli hiyo inafanywa,” alisema Bw Obengo.

Mwenyekiti wa muungano wa NNAK Alfred Obengo akiwahutubia wanahabari katika hospitali ya KNH. Picha/ Magdalene Wanja

Tayari imefichuka kaunti nyingi hazijajiandaa kupambana na homa ya corona endapo ugonjwa huo utaingia nchini kupitia maeneo ya mipaka.

Ni kaunti chache mno, zikiwemo Mombasa, Nakuru, Nairobi, Kisumu, Kitui, Narok na Kajiado ambazo zimetoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na kuzindua hamasisho kuhusu ugonjwa huo hatari.

Kufikia Jumapili, watu zaidi ya 2,000 walikuwa wamefariki ulimwenguni huku wengine zaidi ya 75,000 wakiambukizwa ugonjwa huo ambao ulianzia jiji la Wuhan, China mnamo Desemba mwaka uliopita.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango ya Miji katika Baraza la Magavana, Bw Lee Kinanjui alisema ukosefu wa maandalizi kukabiliana na corona katika kaunti nyingi ni janga linalosubiri kutokea.

“Kaunti nyingi hazijajiandaa kivyovyote licha ya hatari iliyopo. Endapo ugonjwa huo utaingia nchini, basi uchumi wetu utaathirika sana kwa siku moja tu. Ni kama wakazi wameachwa kujitegemea wenyewe,” akasema gavana huyo wa Kaunti ya Nakuru.

Alitoa wito kwa serikali za kaunti ziungane na serikali ya taifa kwa juhudi za kuhamasisha umma na pia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili wajiandae kwa mkurupuko wowote.

“Wanaotazama habari za kimataifa wanafahamu wasiwasi mkubwa hivi sasa ni kuhusu homa ya corona. Lakini hapa Kenya hakuna juhudi kubwa zilizowekwa,” akaeleza.

Serikali ya Kaunti ya Nakuru ilishirikiana na Shirika la Kuzuia Maradhi (CDC) kutoa mafunzo kwa wafanyakazi takriban 70 wa sekta ya utalii kuhusu homa ya corona.

Afisa Mkuu wa Afya katika Kaunti, Dkt Samuel King’ori alisema wamezidisha ukaguzi kwa ushirikiano na wadau wakuu ili kuzuia mkurupuko wa ugonjwa huo hatari.

Wahudumu wa utalii walifunzwa kuhusu jinsi ya kutambua mtu anayeshukiwa kuugua coronavirus na vile wanavyoweza kujiepusha kuambukizwa.

 

Ripoti ya MAGDALENE WANJA, ERIC MATARA na SAMUEL BAYA