PATA USHAURI WA DKT FLO: Tangu mke ajifungue hana haja nami tena
Na DKT FLO
Mpendwa Daktari,
KWA mwaka mmoja sasa nimegundua kwamba mke wangu amekuwa mvivu sana katika masuala ya mahaba. Hafurahii tendo la ndoa kamwe. Tatizo hili lilianza pindi baada ya kuzaliwa kwa mtoto wetu na kusema kweli tatizo hili limeanza kunikera. Nini chaweza kuwa chasababisha tatizo hili na nitafanya nini kurejesha mambo kama yalivyokuwa awali?
Jared, Nairobi
Mpendwa Jared,
Furaha na msisimuko wa tendo la ndoa hutegemea na masuala mengi ya kimwili hasa kwa wanawake. Raha na hamu ya mkeo kwa mahaba vilipungua baada ya kuzaliwa kwa mwanao ambaye hajatimu mwaka mmoja. Wakati huu mtoto huwa na mahitaji mengi, hivyo mkeo huwa amechoka sana wakati ambapo anapaswa kushiriki tendo la ndoa na wewe. Kuna uwezekano mkubwa kwamba bado ananyonyesha na miongoni mwa baadhi ya wanawake, homoni ambazo mwili huhitaji kuzalisha maziwa zaweza kupunguza ashiki. Hofu ya kushika mimba tena pia yaweza kupunguza hamu ya tendo la ndoa. Pia, huenda kuna masuala ya mahusiano au kisaikolojia ambayo huenda yanamuathiri. Itakuwa vyema iwapo utaanzisha mjadala wazi naye kuhusiana na suala hili. Kumbuka kutomhukumu wakati huu. Aidha, litakuwa jambo la busara kuanzisha mjadala huu mahali ambapo hana majukumu (mbali na nyumbani) na uangazie masuala yanayokukera. Pia, waweza kumsaidia na majukumu ya nyumbani kama vile kumshughulikia mtoto ili kumpunguzia uchovu. Mbali na hayo, jifunze mbinu zingine za kumfurahisha mkeo kimahaba pasipo kufanya tendo la ndoa.
Mpendwa Daktari,
Ngozi ya sehemu inayozingira macho yangu imebadilika rangi na kuwa nyeusi. Nitakabiliana vipi na hali hii?
Celine, Nairobi
Mpendwa Celine,
Ngozi ya sehemu inayozingira macho yako inaweza kubadilika rangi na kuwa nyeusi kutokana na sababu mbalimbali. Hii ni pamoja na uchovu, kutopata usingizi wa kutosha, kukaukiwa, anemia, mzio, kujiweka kwenye jua, kuzeeka, uvutaji sigara, kusugua macho, maradhi ya ngozi, maradhi ya tezi au jeni. Tatizo hili hata hivyo halipaswi kukupa wasiwasi ingawa mara nyingi tiba itategemea na vichocheo ambavyo vyaweza kutibiwa kama vile maradhi ya anemia au ugonjwa wa ngozi. Pia, pata usingizi wa kutosha, kunywa maji kwa wingi, usivute sigara au kunywa pombe kupindukia. Kuna krimu za ngozi ambazo huenda zikatumika kurekebisha tatizo hili baada ya kupakwa kwa muda. Tafadhali pata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa ngozi ili upate mawaidha kuhusu mbinu mwafaka ya kukabiliana na shida hii. Kumbuka kuwa pia kuna mbinu za upasuaji ambazo zaweza kutumika kukabiliana na shida hii.
Mpendwa Daktari,
Nina mimba ya miezi sita na ghafla nimekuwa nikitokwa na majimaji kutoka ukeni. Nini chaweza kuwa chasababisha tatizo hili na je ni hatari kwa mtoto wangu ambaye hajazaliwa?
Faith, Mombasa
Mpendwa Faith,
Ni kawaida kwa wanawake hasa baada ya umri wa kubalehe kuanza kutokwa na majimaji ukeni. Hii husaidia kusafisha na kudumisha unyevu katika sehemu hii, na hivyo kuzuia maambukizi. Kwa kawaida mwonekano wa majimaji haya hubadilika kulingana na mzunguko wa hedhi na pia waweza kuathiriwa na mazoezi, msongo wa mawazo, dawa za kihomoni na ashiki.
Ikiwa rangi yake sio ya kawaida (manjano, kijani na wakati mwingine nyeupe), mwasho, harufu mbaya huku majimaji hayo yakiwa yameshikana, basi kuna uwezekano kwamba una maambukizi. Maambukizi haya yaweza kuwa yanasababishwa na ukuvu, bakteria au viumbehai vingine. Hii inapaswa kutibiwa haraka iwezekanavyo kwani ni tishio kwako na ujauzito wako kwani maambukizi haya yanaweza kuenea hadi kwenye uterasi.
Ili kujua nini hasa kinachosababisha tatizo hili, litakuwa jambo la busara kumuona mwanajinakolojia. Ukifika hapa, sampuli ya majimaji haya itachukuliwa na kufanyiwa uchunguzi. Huenda daktari akataka kukufanyia uchunguzi wa mkojo. Pindi baada ya maambukizi haya kutambulika, utapewa dawa na kushauriwa kuhusu cha kufanya siku zijazo. Ikiwa kuna uwezekano wa maambukizi haya kusambaa kupitia tendo la ndoa, basi mwenzako atahitaji matibabu.
Ili kuzuia maambukizi siku zijzao dumisha usafi, unapoenda choo jipanguse kuanzia mbele ukienda nyuma, valia suruali za ndani zilizoshonwa kwa kitambaa cha pamba, jiepushe na mavazi hasa ya ndani yaliyobana, usitumie sabuni na bidhaa zingine za kike zenye harufu kali.