Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tamathali za usemi katika lugha ya kisiasa

March 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na ALEX NGURE

KWA mujibu wa Mulokozi na Kahigi (1979), tamathali za usemi ni vifananisho au viwakilisho vya dhana fulani kwa dhana zingine tofauti au zinazofanana.

Ni usemi wenye kupanua, kupuuza au kubadilisha maana za dhahiri au za kawaida za maneno ili kuleta maana maalum iliyokusudiwa na mtumizi au mzungumzaji.

Tamathali nzuri huyakinisha na kuipa uhai zaidi dhana inayoelezwa;huburudisha na kuzindua akili ya msomaji au msikilizaji na kuacha athari ya kudumu katika hisia na mawazo yake.

CHOMBO

Tamathali za usemi kama tanzu zingine za fasihi simulizi ni chombo cha kutolea mawazo ya jamii; kuibua hisia zao na kukuza ari yao ya kisiasa.Tamathali hutumika katika mazingira halisi ya wanajamii.

Hazitoki katika ombwe tupu. Tamathali za usemi kama tanzu zingine za fasihi simulizi ni chombo cha kutolea mawazo ya jamii. Zinabuniwa na kutumika katika shughuli za kila siku.

Ni dhahiri kuwa lugha hasa ya kitamathali ni chombo madhubuti katika kuhamasisha umma ili uone hali halisi ya mambo ilivyo. Lugha huenda sambamba na mwamko wa kisiasa.

Ni dhahiri kwamba kadiri tunavyokaribia mwaka wa uchaguzi nchini Kenya, tutashuhudia malumbano ya kitamathali yakiibuka katika vyombo mbalimbali vya habari kama vile runinga, redio na magazeti.

Vile vile tutawasikia wanasiasa katika majukwaa ya mikutano ya hadhara, makanisani na hata kwenye hafla za mazishi.wakitoa hotuba zilizosheheni tamathali.

UJUMBE

Mbali na vitendawili na mafumbo,tutawasikia wanasiasa wakitumia methali kuwasilisha ujumbe wao wa kisiasa. Wanasiasa wametambua kuwa huu ni utanzu mwafaka wa kutolea ujumbe wao na kuhamasisha umma kuwaunga mkono.

Wairagu (2001)anasema kuwa baadhi ya maoni na mawazo, hasa yale yanayolenga hisia za hadhira hufaa zaidi yakitolewa kwa njia ya methali na jazanda.

Mojawapo ya methali inayotumiwa sana katika kumbi za siasa ni: Nyani haoni kundule.Aghalabu methali hii hutumiwa kuashiria ukweli kwamba baadhi ya viongozi ambao daima huwashutumu wenzao kwa uozo huu ama ule; wao wenywewe wanaendeleza au wamewahi kuhusika na uozo ule ule.

UFANANISHO

Tamathali za ufananisho kama vile tashbihi,sitiari,jazanda na tabaini zimetumika kwa mapana na marefu katika kumbi za siasa.Katika matumizi haya,tabia za baadhi ya viongozi zimelinganishwa na wanyama.Kwa mfano,nguruwe ama fisi wametumiwa kudhihirisha ulafi wa baadhi ya viongozi.

Baadhi ya viongozi wamelinganishwa na ngiri-mnyama ambaye husahau haraka sana. Neno kinyonga hutumiwa kuashiria viongozi ambao hawana msimamo dhabiti wa kisiasa. Wengine huwaita tikiti-maji (water-melon). Hili ni dhihirisho la misimamo ya kuyumba yumba ya baadhi ya viongozi ambayo, aghalabu huwapotosha wafuasi wao.Hali hii imewafanya baadhi ya viongozi kulinganishwa na panya vipofu ambao hawatoi mwelekeo ufaao kwa wafuasi wao.

MAFUMBO

Mafumbo pia ni mbinu ya kitamathali ambayo inatumiwa na wanasiasa kuelimisha wananchi ili waweze kuelewa mazingira yao ya kisiasa.

Mfano wa fumbo ni kama hili:kupaka rangi nyumba si kugeuza.

Fumbo hili limetumika kuonyesha kwamba wanaopania kuondoa utawala ulioko na kuleta utawala mpya ni sawa na kupaka nyumba rangi ambako mbali na kuwa katika sura mpya,hakutatokea mabadilko yoyote ya haja.

Mfano mwingine unaofafanua dhana hii ni ule unaosema:msitu umebadilika lakini nyani ni wale wale.

Inadaiwa kwamba malumbano ya kitamathali yalichangia pakubwa kutokea kwa machafuko yaliyotishia kuliangamiza taifa hili baada ya uchaguzi wa 2007.

Inasemekana matumizi ya maneno kama vile ‘kwekwe’ na ‘madoadoa’ miongoni mwa tamathali nyingine,yalichangia pakubwa katika kufurushwa kwa baadhi ya jamii kutoka maeneo fulani ya Kenya.

Mchanganuzi mmoja wa maswala ya kisiasa anasema: ’Kwa bahati mbaya, machafuko haya yalibadilisha mwelekeo; mkondo mzima wa kisiasa;maingiliano na mahusiano ya Wakenya na kuacha taathira itakayodumu kwa muda mrefu, hususan kwa watoto walioshuhudia yaliyotokea’

Kwa bahati mbaya inaonekana kama kwamba Wakenya hawakujifunza lolote kutokana na machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

UTANGAMANO

Kwa mfano, inadaiwa kuwa kusudi la BBI ni kuwaunganisha Wakenya. Iwapo kuna ukweli katika madai haya, basi siasa za BBI hazina budi kuendeshwa kwa kusudi la kuimarisha utangamano na uwiano wa kitaifa.

Kwa upande mwingine, tumeshuhudia nyimbo na hotuba za uchochezi unaoweza kuhatarisha amani ukiendeshwa katika mitandao ya kijamii.

Baadhi ya jumbe zinazotolewa katika mitandao ya kijamii hazichangii kwa vyovyote vile katika kuimarisha umoja wa kitaifa.

Tume ya uwiano wa kitaifa haina budi kuwachukulia hatua kali wachochezi hawa wasije wakalitumbukiza taifa hili katika lindi la maangamizi.