• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
SEKTA YA ELIMU: Serikali yarundika wanafunzi shuleni bila ya pesa za kutosha kuajiri walimu

SEKTA YA ELIMU: Serikali yarundika wanafunzi shuleni bila ya pesa za kutosha kuajiri walimu

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine mpango wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) wa kuajiri walimu zaidi kupunguza tatizo la uhaba wa walimu umegonga mwamba baada ya Wizara ya Fedha kupunguza mgao wa fedha za kufadhili shughuli hiyo.

Ni kinaya kwamba wiki iliyopita Wizara ya Elimu ilitangaza kwamba asilimia 99. 8 ya wanafunzi waliofanya mitihani wa kitaifa wa darasa la nane wamejiunga na kidato cha kwanza, ilhali hamna walimu wa kutosha kuwafunza.

Kulingana na Taarifa kuhusu Sera ya Bajeti (BPS) ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021 unaoanza Julai mwaka huu, TSC imetengewa Sh3.2 bilioni pekee za kuajiri walimu ilhali tume hiyo iliomba Sh20.2 bilioni.

Waziri wa Fedha Ukur Yatani amesema hatua hiyo imechangia na kupungua kwa mapato ya serikali ya kitaifa huku ikilazimika kulipa madeni yake ya kigeni kwa wakati uliowekwa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Nancy Macharia aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kwamba pengo la Sh17 bilioni katika bajeti yake ya kuajiri walimu itaathiri pakubwa mipango yake ya kuajiri walimu watakaofanikisha sera ya Elimu Bila Malipo (FPE) katika shule za msingi.

Vile vile, akaongeza, mpango wa serikali wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) wanajiunga na shule za upili utaathirika pakubwa.

“Tume ilipanga kutumia Sh4.8 bilioni kuajiri walimu 40,000 vibarua na walimu 25,000 na Sh15.4 bilioni kuajiri walimu 25,000 kwa mkataba wa kudumu. Lakini sasa hatutaweza kufikia azma hii inayolenga kupiga jeki mpango wa elimu kwa wote,” Dkt Macharia akawaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao, Mbunge wa Tinderet Julius Melly.

Alikadiria kuwa mgao wa Sh3.2 bilioni utaiwezesha TSC kuajiri na kuwalipa walimu 5,000 wapya pekee na vibarua 10,000 kati ya Julai mwaka huu hadi Juni 30, 2021.

Mwaka jana, bunge la kitaifa liliagiza TSC kuajiri jumla ya walimu 80,000 kama vibarua sehemu za hatua ya kupunguza kero la uhaba wa walimu katika shule za msingi na za upili za umma. Lakini hiyo haitewezekana sasa.

Takwimu kutoka TSC zinaonyesha kuwa shule za msingi na za upili zinakabiliwa na uhaba wa takriban walimu 120,000. Na kufikia sasa tume hiyo imesajili jumla ya walimu 180,000 zaidi waliohitimu lakini hawana ajira.

Hata hivyo, wabunge waliitaka, TSC kuelekeza kiasi fulani cha fedha ilizotengewa kwa ajili ya kufadhili miradi ya maendeleo kwa mpango wa uajiri wa walimu wapya. Katika bajeti ijayo TSC imetengewa Sh60 bilioni za kufadhili miradi ya maendeleo.

“Bajeti inastahili kulipa uzito suala la uajiri wa walimu. Tunataka kujua idadi ya walimu ambao wataajiriwa katika shule za msingi, shule za upili na vyuo vya kadri, Na ninaunga mkono pendekezo la mwenyekiti wangu kwamba walimu hao waajiri kwa mkataba wa kudumu sio vibarua,” akasema Mbunge Maalum Wilson Sossion.

Walimu 6,000 kati ya walimu 10,000 vibarua walioajiriwa Januari mwaka huu walitumwa kufunza katika shule za msingi huku 4,000 waliosalia wakatumwa kwa shule za upili.

Wale wanaofunza katika shule za msingi wanalipwa Sh10, 000 kwa mwezi huku wenzao wanaofunza katika shule za upili wakilipwa Sh15, 000. Kiasi hicho cha malipo hutozwa ushuru wa mapato wa asilimia 30.

Wakati huo huo, Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang’ aliwataka wabunge kutenga fedha za kutosha kwa wizara hiyo kufadhili mpango wa utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu (CBC).

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Mbona ananihadaa kuwa ana mke na watoto?

Mahakama yatupa ombi la Aukot la kutaka jopokazi la BBI...

adminleo