NDIVYO SIVYO: Si wakati wote neno 'kuhusu' humaanisha 'kwa sababu'
Na ENOCK NYARIKI
AGHALABU kihusishi ‘kuhusu’ hutumiwa kuandika vichwa vya habari hasa kwenye magazeti.
Katika miktadha kadha, kihusishi hicho hudhaniwa kuwa na maana sawa na ‘kwa sababu’.
Tazama kilivyotumiwa visivyo katika kichwa kimojawapo cha habari: ‘Waziri mkuu atakiwa kujiuzulu kuhusu mauaji’. Nitafafanua zaidi kwa nini kichwa hiki si sahihi ila nitaje hapa kuwa neno hilo linapotumiwa kwa maana ya ‘kwa sababu’, lengo la mwandishi wa kichwa cha habari huwa ni kutumia iktisadi ya maneno. Yaani, badala ya kuyatumia maneno mawili ambayo ni ‘kwa’ na ‘sababu’, neno kuhusu linaweza kutumiwa hivyo basi kufidia vyema nafasi iliyotengewa kichwa cha habari. Upotoshi ulioje!
Kamusi ya Karne ya 21 inaeleza kuwa dhana kuhusu ina maana ya ‘juu ya’. Ingawa kwa kiwango fulani maneno ‘juu ya’ yanaweza kutumiwa kama kiunganishi kwa maana ya ‘kwa sababu’, kwa mujibu wa kamusi tuliyoitaja, yametumiwa kama kihusishi kurejelea mada, uwanja au suala lolote lililojikita katika mazungumzo au maandishi.
Mfano: Shisia ameandika hadithi fupi kuhusu uzandiki. Katika sentensi hii neno hilo limetumiwa kwa maana ya mada ambayo Shisia ameandika juu yake. Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza inatafsiri kuhusu kama ‘about’.
Waama, kuchukulia kuwa neno kuhusu lina maana sawa na kwa sababu au kutokana na ni sawa na kudai kuwa neno la Kiingereza ‘about’ lina maana sawa na ‘because’.
Kwa hivyo waandishi wa habari wanapoandika: ‘Ameshtakiwa kuhusu ufisadi’; ‘Amefungwa jela kuhusu ubadhirifu wa pesa za umma’, vichwa hivyo vinapotosha kwa sababu neno mwafaka linalopaswa kutumiwa katika muktadha huo ni ‘kwa sababu’. Neno ‘kwa sababu’ linaonyesha chanzo au kinachochochea kutendeka kwa jambo fulani.
Sasa turudi katika kichwa tulichokitaja katika utangulizi wa makala: Waziri mkuu atakiwa kujiuzulu kuhusu mauaji. Ujumbe muhimu ambao unapaswa kujitokeza katika kichwa hiki ni sababu zinazowafanya watu kumshinikiza waziri mkuu kujiuzulu. Jambo hilo halijidhihirishi wazi kwenye kichwa. Kichwa hiki kikitafsiriwa moja kwa moja hadi lugha ya Kiingereza kwa kutumia neno ‘about’ hakitakuwa na maana yoyote.
Alhasili, neno kuhusu halina maana sawa na ‘kwa sababu’ wala halionyeshi chanzo au kichocheo cha kutendeka kwa jambo fulani . Kuhusu ni kihusishi ambacho hutumiwa kuonyesha mada au suala lolote linalorejelewa katika mazungumzo. Waandishi wa habari wanapolitumia kimkato kama njia moja ya kutumia iktisadi ya maneno katika kuandika vichwa vya habari wanaupotosha ukweli wa mambo