Habari Mseto

Wanaharakati wataka serikali ieleze jinsi itakavyohifadhi mazingira wakati wa ujenzi wa barabara ya Expressway

March 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA 

WANAHARAKATI wa mazingira wametaka uwazi kutoka kwa serikali katika mpango wa ujenzi wa barabara kutoka katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi Westlands ambayo itafahamika kama Expressway.

Hii ni baada ya mipango ya ujenzi wa barabara hiyo kuanza upya licha ya pingamizi kutoka kwa vitengo mbalimbali.

Wanaharakati hao walizungumza katika eneo la Freedom Corner wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Barani Afrika ambapo pia mwanaharakati marehemu Profesa Wangari Maathai hukumbukwa.

Kuanzia mwaka 2012, sherehe hiyo hufanyika Machi 3 kumkumbuka Maathai ambaye alipigania uhifadhi wa mazingira.

Bi Wanjira Maathai ambaye ni naibu wa rais na mkurugenzi wa eneo la Afrika katika Taasisi ya Raslimali za Dunia – World Resources Institute – alisema kuwa ni muhimu serikali kuwa wazi na kuwahusisha wananchi ambao ndio wataathirika sana na mradi huo.

“Iwapo serikali itachangia katika kuharibu bustani ya Uhuru Park, utakuwa mwanzo wa uharibifu zaidi wa mazingira muhimu kwa binadamu na hasa katika miji mikuu,” akasema Wanjira Maathai.

Wanamazingira hao wanahofia kuwa mradi huo utaharibu bustani ya Uhuru Park ambayo iko katikati mwa jiji la Nairobi.

Mwenyekiti wa shirika la Greenbelt Movement Bi Marion Kamau alielezea hofu yake kuhusu jinsi ambavyo baadhi ya bustani zimenyakuliwa na kuharibiwa licha ya juhudi za kuhifadhi kutoka kwa wanamazingira.

Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko katika taarifa iliyosomwa na msimamizi wa uhifadhi misitu – Chief Conservator – Bw Julius Kamau alisema kuwa serikali inanuia kupanda miti 360 milioni kila mwaka kufikia mwaka 2022.