Raila si mganga, viongozi wa dini wamkanya Ruto
Na JUSTUS OCHIENG’
VIONGOZI wa kidini kutoka eneo la Nyanza wamemkashifu Naibu Rais, Dkt William Ruto kwa kumrejelea Kinara wa ODM Raila Odinga kama mganga, wakisema kigogo huyo wa upinzani ni Mkristo mcha Mungu.
Kupitia Baraza la Viongozi wa Makanisa eneo la Nyanza, viongozi hao walisema hawataendelea kuvumilia matamshi makali ya Naibu Rais dhidi ya Bw Odinga wakimtaka akome na kuridhiana naye kisiasa iwapo anahitaji uungwaji mkono wake 2022.
Mwenyekiti wa Baraza hilo Askofu Dkt Washington Ogonyo-Ngede na Naibu wake Askofu Julius Otieno walisema Bw Odinga ni Mkristo aliyebatizwa huku pia wakitetea matamshi yake ya kuwakashifu viongozi wanaotoa michango mikubwa makanisani.
Aidha walimkumbusha Dkt Ruto kuhusu kitabu cha Mathayo 7: 21 kinachosema “Si kila mtu aniitaye bwana ataingia kwenye ufalme wa mbinguni, ila afanyaye mapenzi ya babangu aliye mbinguni.”
Pia walimkumbusha Naibu Rais asome kitabu cha Luka 18 9-14 kinachozungumzia Wafarisayo na mtoza ushuru.
Dkt Ruto amekuwa akivamia Bw Odinga mara kwa mara kwa kumrejelea kama mganga huku Waziri huyo mkuu wa zamani naye akimwita kuhani mkuu wa ufisadi nchini.
Vilevile taarifa ya maaskofu hao ilitetea matumizi ya muziki wa reggae katika mikutano ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) wakisema nyimbo hizo zinatumika kuwasilisha ujumbe wa kisiasa badala ya madai ya Dkt Ruto kuwa muziki huo unapotosha.
“Wakati wa siasa, viongozi wapo huru kutumia lugha yoyote wanayoona inafaa. Nyimbo za reggae zinatumika kuwasilisha ujumbe wa kisiasa wala sio kumdunisha Mungu jinsi anavyodai Dkt Ruto,” ikasema taarifa yao.
Aidha walisema umefika wakati ambapo Dkt Ruto anafaa akome kumhusisha Bw Odinga na uganga kwa sababu yeye ni binadamu na hana mamlaka ya kuamua mtu anayemwamini Mungu ama yule anayemwabudu shetani.
Kwa kauli moja, walitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono ushirikiano kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta maarufu kama ‘handisheki’ wakisema ukuruba kati ya wawili hao umehakikisha amani inadumu nchini.
“Hatutaki BBI imalizwe na baadhi ya wanasiasa ambao hawako tayari kuona kama Wakenya wameungana. Wanasiasa kutoka mirengo yote wanafaa wahakikishe kwamba semi zao hazichochei raia kikabila na kuzua mgawanyiko,” akasema Askofu Otieno.
Viongozi hao wa kanisa sasa wanaungana na wabunge wa ODM na wale wa mrengo wa Tangatanga ambao wamekuwa wakikemea matamshi yaliyotolewa na Naibu Rais kuwa atahakikisha mikutano ya BBI inasitishwa akidai inatumika kuhubiri chuki na kuchochea makabila mbalimbali.
Wabunge Joshua Kuttuny (Cherangany), Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na mbunge wa Nyeri Ngunjiri Wambungu, ni kati ya viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea mikutano ya BBI wakisema Dkt Ruto hawezi kamwe kusimamisha ‘reggae’.
“Anafaa ajitokeze hadharani na kusema anapinga BBI badala ya kujificha kwa kutumia masuala madogo madogo kama nyimbo. Mikutano ya BBI inaweza kusimamishwa na Raila na Uhuru pekee yao,” akasema Bw Kuttuny.