• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
Kampeni kuangazia funza

Kampeni kuangazia funza

Na CHARLES LWANGA

KAMPENI ya kukabiliana na funza nchini itachukuwa mkondo mpya na kuanza kutoa huduma kabambe za afya baada ya kuhamasisha takriban asilimia 95 ya wananchi.

Afisa mkuu mtendaji wa shirika la Ahadi Kenya Trust Foundation, Dkt Stanley Kamau, akiandamana na maafisa wa afya, alisema wahudumu wa afya wa kujitolea hawatafanya kampeni ya nyumba hadi nyumba pekee bali pia watatibu maradhi mengine ambayo yanaathiri wakazi.

Alikuwa akizungumza katika eneo la Msahaba-Malindi wakati wa sherehe za kuidhinisha siku ya kuhamasisha watu jinsi ya kukabiliana na funza nchini

Alisema lengo la kutoa huduma zingine za afya ni kuwawezesha wakazi kujitegemea na kutibu madhara yanayoletwa na funza.

“Kuna maafa mengi ambayo hukumba familia ambazo zimeshambuliwa na funza kwa sababu watoto wao mara nyingi huchelewa kupata chanjo, huku wengine wakikosa chanjo ya homa ya mapafu na malezi bora utotoni kutokana na umaskini,” alisema.

Shirika hili limekuwa likifanya kampeni ya kukabiliana na funza kwa miaka 13 iliyopita.

Dkt Kamau alisema ingawa kampeni ya kukabiliana na funza nchini haijapokea msaada kutoka kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), serikali ilizindua sheria mnamo 2015 ambayo inasaidia kuzuia makali ya funza, ambayo imefanya kampeni yao kufaulu.

“Funza hazibagui kabila, mipaka, dini wala rangi ya ngozi, vile vile, hazibagui ikiwa mtu ni kijana, mzee au mtoto kwa sababu zinaathiri mtu yeyote,” akasema.

Pia, aliwahimiza Wakenya wakumbatie kampeni hiyo kwa kutowatenga wale ambao wameathirika na funza.

Wakati wa sherehe hiyo ambayo ilipangwa na Shirika la Imarika kupitia kitengo chao cha afya, mamia ya wakazi ambao walienda kupokea matibabu ya funza pia walipokea huduma ya afya bila malipo.

Bw John Kipsiwa, Naibu Kamishna wa Malindi aliwasihi wadau waungane mkono ili wakabiliane na janga la funza katika jamii.

“Tungane ili tutembelee wakazi ambao wameshindwa kutoka nyumbani kwao kupata matibabu kwa zahanati kutokana na athari za funza. Vile vile, tuwasaidie wale ambao wanaogopa kujitokeza kutokana na aibu,” alisema Bw Kipsiwa.

Waliohudhuria sherehe hiyo ni: Renson Ndoro, mwenyekiti wa shirika la Imarika, Bernadette Mwikali, mwakilishi wa Kenya AIDS NGOs Consortium (KANCO) na aliyekuwa Bi Kenya na Ulimwengu, Bi Cecelia Mwangi na wengineo.

You can share this post!

Raila si mganga, viongozi wa dini wamkanya Ruto

Wafisadi wahukumiwe kifo – Wetangula

adminleo