CORONA: Maelfu kupoteza ajira
Na BENSON MATHEKA
MAELFU ya Wakenya wako katika hatari ya kupoteza kazi na mapato ikiwa maambukizi ya virusi vya corona yataendelea kuenea ulimwenguni.
Bei ya bidhaa pia inatarajiwa kupanda kwani biashara nyingi nchini yakiwemo maduka makubwa na wachuuzi hutegemea bidhaa kutoka China ambako maradhi hayo yalianzia mwaka jana.
Uhaba wa bidhaa umesababishwa na viwanda vingi ambavyo wafanyabiashara wa Kenya wamekuwa wakinunua bidhaa nchini China kufungwa.
Safari za ndege kutoka China na nchi zilizoripoti visa vya virusi vya corona nazo zimesimamishwa na kuathiri usafirishaji bidhaa pamoja na sekta ya utalii ya Kenya.
Wadau katika sekta ya utalii wanasema safari za ndege zimesitishwa maeneo wanakotoka watalii wengi wanaotembelea Kenya hasa China na Italia.
Hii imesababisha hofu miongoni mwa vijana na wafanyabiashara wanaotegemea utalii wa kupoteza kazi na mapato.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa chama cha wenye hoteli nchini Mike Macharia, wadau wanatafuta mbinu za kuepusha hasara inayoweza kusababishwa na maradhi hayo.
Tayari idadi ya watu wanaosafiri kwa ndege imepungua kwa asilimia sita kufuatia athari za maradhi hayo.
Mwenyekiti wa maajenti wa safari za ndege Mohammed Nyoike anasema idadi hii inaendelea kupungua.
Katika sekta ya kilimo, wakulima wa kahawa, majani chai na parachichi wameathirika baada ya safari za ndege kwenda China kusimamishwa na hivyo kuwaweka katika hatari ya kupoteza kazi na mapato.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wadogo wadogo jijini Nairobi Samuel Karanja, anasema Wakenya wanafaa kujiandaa kwa maisha magumu ikiwa ni pamoja na uhaba wa bidhaa na kupanda kwa bei ikiwa maradhi hayo hayatakabiliwa karibuni.
Maduka makubwa ya Naivas na Tusky’s tayari yametoa tahadhari kuwa bei za bidhaa zitaongezeka.
Maduka hayo yanasema yatakubwa na uhaba wa bidhaa kutokana na maradhi hayo na kulazimika kupandisha bei za baadhi ya bidhaa.
Miongoni mwa bidhaa zinazouzwa jijini Nairobi zikiwemo simu, bidhaa za urembo, vifaa vya nyumbani, kieletroniki na fanicha huwa zinatoka China.
“Tumefahamishwa kuwa kutakuwa na uhaba wa bidhaa na tunatarajia bei ya bidhaa itaongezeka,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa maduka ya Tuskys Dan Githua.
Peris Kioko, muuzaji wa simu katika barabara ya River Road jijini Nairobi anasema amelazimika kuongeza bei kwa kati ya asilimia 10 na 20 kuanzia mwezi uliopita.
“Sio kupenda kwetu. Hata sioni tukiendelea na biashara kwa sababu bidhaa haziingii nchini. Wenzangu wengi wamefunga kazi,” akasema
Bandari nchini China kadhaa zimefungwa hatua ambayo inatarajiwa kuathiri sekta ya uchukuzi hasa biashara ya vipuri vya magari ambavyo husafirishwa kwa meli.
Hii inaweza kusababisha uhaba wa vipuri vya magari na mashini zinazotumiwa viwandani na hivyo kulemaza huduma.
Mnamo Jumatatu, Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) iliambia gazeti la East African kwamba idadi ya meli zinazoleta bidhaa kutoka China imepungua na hali hiyo inatarajiwa kuendelea.
Ben Kamau, mmoja wa waagizaji wa bidhaa, aliambia Taifa Leo kuwa anategemewa na wachuuzi 140 kote nchini lakini kwa sasa hana bidhaa za kuwauzia.
Alisema tangu mkurupuko wa maradhi ya corona hajaweza kuagiza bidhaa kutoka China.
“Hali ikiendelea hivi, uchumi wa Kenya utakwama. Maradhi haya yakiendelea, maduka mengi eneo la Kirinyaga, Kamukunji na River Road yatafungwa,” akasema Bw Kamau.