• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
TEKNOHAMA: Simu inaweza kueneza homa ya Corona

TEKNOHAMA: Simu inaweza kueneza homa ya Corona

Na LEONARD ONYANGO

SIMU yako huenda ikakufanya kupata maambukizi ya homa ya Corona ambayo imeua karibu watu 3,700 na kuambukiza wengine 108,000 kote duniani, wataalamu wameonya.

Japo muda ambao virusi vya corona vinaweza kuishi kwenye simu bado haujulikani, matokeo ya utafiti uliochapishwa katika jarida la ‘Journal of Hospital Infection’ unasema kuwa sawa na viini vinginevyo vinavyosababisha magonjwa, virusi vya corona vinaweza kuishi kwenye skrini au sehemu yoyote ya simu kwa takribani siku tisa.

Naye daktari mtajika nchini Uingereza Profesa Chris Whitty anasema kuwa virusi vya corona vinaweza kuishi katika eneo gumu kama vile simu, mti au chuma kwa takribani siku tatu.

Wizara ya Afya nchini Uingereza inasema kuwa virusi vya corona vinakufa ndani ya saa 48 vinapokuwa nje ya mwili.

Virusi vya corona huingia mwilini ikiwa mtu atagusa mwathiriwa au kitu chenye virusi na kisha kugusa mdomo, pua au macho.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa itakuwa kazi bure iwapo utanawa mikono kuepuka virusi vya corona na kisha kuendelea kutumia simu chafu.

Maski mdomoni

Mkurugenzi wa Matibabu wa Singapore, Kenneth Mak, wiki iliyopita aliambia raia wa nchi hiyo kuwa kusafisha simu ni muhimu kuliko kuvalia maski mdomoni kuzuia virusi vya corona kuingilia mdomoni au puani.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa zimebaini kuwa simu imesheheni zaidi ya viini 25,000 vinavyosababisha maradhi.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Arizona, Amerika ulibaini kuwa viini vinavyopatikana kwenye simu ni mara 10 zaidi ya vile vilivyoko chooni.

Watafiti hao pia walibaini kuwa kwa wastani mtu hushika simu yake mara 47 kwa siku.

Serikali ya China, mwezi uliopita ilianzisha operesheni ya kuharibu fedha (noti na sarafu) kama njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Ikiwa virusi hivyo vinaweza kuenezwa kupitia fedha, wataalamu wanasema, kuna uwezekano pia kwamba vinaweza kusambaa kupitia simu chafu.

Wataalamu wanasema kuwa hata ikiwa simu yako unaitumia peke yako bila kuguswa na wengine ni vyema isafishwe.

Jinsi ya kusafisha simu

Wataalamu wanashauri kuwa usafishe simu yako kwa kutumia maji na sabuni ya kawaida. Lakini kabla ya kutumia maji ni sharti ufahamu ikiwa simu imetengenezwa kwa teknolojia inayoruhusu maji kuingia ndani au la.

Kadhalika, unaweza kutumia sabuni spesheli iliyotengenezwa kwa ajili ya kusafishia skrini za simu.

Epuka kutumia kemikali ambazo huenda zikaharibu skrini.

Mbali na simu, wataalamu wanasema kuwa fedha pia zinaweza kusambaza virusi vya corona kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Kunawa mikono

Wataalamu wanashauri kuwa ni vyema kunawa mikono vizuri baada ya kushika fedha ili kuepuka kupatwa na virusi vya corona.

Manyoya ya mbwa, paka au mbuzi, farasi, punda kati ya mifugo mingine pia yanaweza kueneza virusi vya Corona iwapo wanyama hao wataguswa na mwathiriwa.

Mwathiriwa wa homa ya Corona hutoa chembechembe za virusi vya maradhi hayo anapozungumza, kupumua, kucheka na hata kupiga chafya. Virusi hivyo husafiri hewani na kuambukiza watu walio karibu.

Virusi vya corona vinaweza kusalia hewani kwa zaidi ya dakika 10, kulingana na wataalamu.

Hiyo inamaanisha kwamba, ikiwa mwathiriwa wa virusi vya corona alipiga chafya ndani ya lifti au matatu na akashuka na mtu mwingine akaingia ndani ya dakika 10, basi yuko katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo.

Wataalamu wanaamini kuwa mwathiriwa anaweza kusambaza virusi vya maradhi hayo hata kabla ya kuonyesha dalili.

You can share this post!

LSK yapinga pendekezo la Kaluma kwenye mswada wake wa...

MAZINGIRA NA SAYANSI: Hewa chafu inakupunguzia hadi miaka 3...

adminleo