• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Wafungwa 130 katika gereza la Thika watuzwa vyeti elimu ya Biblia

Wafungwa 130 katika gereza la Thika watuzwa vyeti elimu ya Biblia

Na LAWRENCE ONGARO

GEREZA limetajwa kama mahali pa kurekebisha tabia na kupalilia matendo mema wala sio mahali pa kuadhibiwa.

Mkurugenzi mkuu na Rais wa shirika la kiroho la Prison Fellowship International Bw Andrew Corley, amesema wafungwa wanastahili kumweka Mungu mbele ili aweze kuwafungulia njia ya matumaini katika siku za baadaye.

Amesema yeyote aliye gerezani anastahili kuweka maombi mbele kwani kufungiwa huko sio mwisho wa maisha, kwa sababu kuna maisha mengine ya kutegemewa na ni hasa ya kidini.

Ameyasema hayo Jumanne katika gereza kuu la Thika wakati wafungwa wapatao 100 wa kiume na 30 wa kike wamefuzu katika masomo ya dini na kiroho waliyopitia katika gereza hilo.

Wakati wa hafla hiyo wafungwa hao wamepokea vyeti maalum, Biblia, nguo, viatu, sabuni ya kuogea, maziwa na mikate huku wakipewa matumaini kuhusu maisha ya baadaye.

“Mimi kama mtumishi wa Mungu nimefika hapa kuwafariji na kuwapa matumaini ili mtakapotoka nje muweze kuwa watu waaminifu wa kutegemewa na umma. Kwa hivyo, ni vyema kumweka Mungu mbele ili kuwa kama ngome yako katika maisha,” amefafanua Bw Corley.

Mkurugenzi wa Shirika la Prison Fellowship International Bw Andrew  Corley ahutubia wafungwa wa gereza la Thika wakati wa kuwapa vyeti wale waliofuzu. Picha/ Lawrence Ongaro

Amesema kwa kipindi cha miezi michache amezuru nchi kadha za bara la Afrika nazo ni Zambia, Zimbabwe, Botswana, na sasa yumo nchini Kenya.

Amesema shirika lake lina matawi 112 ulimwenguni kote, na lilibuniwa miaka 40 iliyopita na ameweza kuzuru nchi kadha na kujionea mwenyewe jinsi maisha ya wafungwa yanavyoendeshwa.

“Yeyote aliye gerezani ana mawazo mengi akilini kwa sababu kupata uhuru ni jambo linalohitaji busara kweli. Aliye gerezani ni mtu ambaye anapitiwa na mawazo mengi ambayo yanaweza hata kumkosesha usingizi,” amesema Bw Corley.

Alisema hapa nchini wanafanya kazi kwa karibu na magereza 70 ambapo wafungwa wanapata mafunzo kupitia shirika hilo.

Amezidi kufafanua kuwa kuna magereza 330,000 kote ulimwenguni ambayo wanahusiano nayo kupitia mafunzo ya kiroho na kidini.

“Sisi pia hutembelea jamii tofauti mashinani ili kuwalisha neno la Mungu na kuwapa matumaini zaidi,” amesema.

Afisa mkuu wa gereza la Thika Bw Billy Koshal, amesema mpango huo wa kuwapa masomo ya dini wafungwa ni hatua nzuri ambayo inarekebisha mienendo yao na fikira.

“Hata hapa gerezani tuna wataalamu ambao wanawapa mafunzo wafungwa ambao wangetaka kujiendeleza zaidi na masomo yao. Hata masomo ya ngumbaru yanaendeshwa hapa kwa wale wangetaka kujua kusoma na kuandika kwa manufaa yao wenyewe,” amesema Bw Koshal.

Alisema baada ya wafungwa wengi kuhamasishwa kuhusu hali yao ya maisha wengi hutoka wakiwa wamejirekebisha kabisha na wenye nidhamu ya hali ya juu.

Amesema changamoto kuu wanayopitia ni wafungwa kurundikana gerezani ambapo mahabusu ambao vifungo vyao havijapitishwa ndio wengi.

“Jambo hilo ni changamoto kubwa kwetu tukilinganisha na wafungwa halisi walio mahali hapo. Makosa madogo yanastahili kutatuliwa nje ya mahakama ili kusiwe na msongamano mkubwa gerezani,” amesema afisa huyo.

You can share this post!

Murkomen alalama Dkt Ruto kapokonywa majukumu...

Majonzi tena kansa ikimuua mbunge Suleiman Dori

adminleo