• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
Raila hafai kugombea urais 2022 – Kalonzo

Raila hafai kugombea urais 2022 – Kalonzo

Na WANDERI KAMAU

KINARA wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka amesema kuwa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga hapaswi kuwania urais mnamo 2022, kwani ametetea sana uwepo wa demokrasia nchini.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni mnamo Jumapili usiku, Bw Musyoka alisema kwamba itakuwa busara kwa Bw Odinga kutathmini mwelekeo mwingine kisiasa, ikizingatiwa amewania urais mara nne bila mafanikio.

“Sote tu binadamu. Ikiwa atawania urais wakati huo [2022] basi itakuwa mara yake ya tano. Imefikia wakati atathmini mwelekeo mpya kisiasa, kwani amepigania sana uwepo wa demokrasia nchini, kiasi kwamba harakati hizo wakati mwingine zimemgeuka,” akasema.

Bw Musyoka alimuunga mkono Bw Odinga kuwania urais mnamo 2013 na 2017 kama mgombea-mwenza, ingawa hawakuibuka washindi.

Wawili hao waliwania nafasi hiyo kwa tiketi za mirengo ya Cord na NASA mtawalia. Kabla ya hapo, Bw Odinga aliwania urais mnamo 1997 na 2007, ambapo pia hakuibuka mshindi.

Na ijapokuwa Bw Musyoka amesema kuwa atashirikiana kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta, alisema kuwa hilo halimaanishi kwamba ataunga mkono chaguo lake kuhusu yule atakayewania urais.

“Ni kweli nimetangaza nitashirikiana na Rais Kenyatta hata baada ya 2022. Hata hivyo, hilo halinizuii kumkosoa, ikiwa nitahisi chaguo lake haliniridhishi,” akasema.

Bw Musyoka alieleza kuwa kauli yake haimaanishi kwamba yeye ni hasimu wa Bw Odinga, lakini anatoa kauli ambayo anahisi inamfaa zaidi.

Tofauti za kisiasa ziliibuka kati yake na Bw Odinga baada ya kukosa kuhudhuria hafla ya kumwapisha Bw Odinga kama “Rais wa Wananchi” mnamo Januari 30, 2018 katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi.

Bw Musyoka alikosa kuhudhuria hafla hiyo pamoja na kinara wa ANC Bw Musalia Mudavadi na kiongozi wa Ford-Kenya Bw Moses Wetang’ula, kwani walikuwa vinara-wenza katika NASA.

Kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI), Bw Musyoka alisema kuwa mikutano yake haipaswi kugeuzwa kuwa mjadala kuhusu nafasi ya viongozi, ili kuhakikisha kuwa unazingatia mahitaji ya Wakenya.

Alisema pana haja kwa viongozi kuzingatia ukweli, ili kuhakikisha kuwa Kenya haijakumbwa na ghasia kama Sudan Kusini.

“Katika kiwango ambacho ripoti ya BBI imefikia, ni lazima viongozi wajihadhari sana kuhakikisha kuwa mchakato huo haujatekwa na matakwa yao binafsi. Hili litahakikisha kuwa wananchi wamepata nafasi nzuri kueleza kiwazi changamoto zinazowakumba bila kuogopa,” akasema.

Baadhi ya wabunge wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao unamuunga mkono Naibu Rais Wiliam Ruto, wamekuwa wakiteta kwamba mchakato wa ripoti hiyo umetekwa na ODM.

Wanasema kuwa mikutano hiyo imegeuzwa jukwaa la kumfanyia kampeni Bw Odinga kwenye azma yake ya urais mnamo 2022.

You can share this post!

Msijaribu kuvuruga BBI Afraha, Tolgos aonya Tangatanga

City Stars yaangusha APs Bomet BNSL

adminleo