Makala

NGILA: Tutumie teknolojia kuzuia maambukizi ya corona

March 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTINE NGILA

KWA miezi miwili sasa, nimekuwa nikifuatilia kwa karibu jinsi ambavyo mataifa mbalimbali duniani yamekuwa yakikabiliana na kuenea kwa virusi vya corona ambavyo kwa sasa vimezua zaidi ya vifo 3,600.

Mbali na mataifa yanayoendelea mathalani Kenya, mataifa mengi duniani yanategemea uwezo wa teknolojia katika kupunguza maambukizi mapya.

Nimebaini kuwa miongoni mwa teknolojia inayotumiwa zaidi ni Intelijensia Bandia (AI), kutokana na uwezo wake wa kuunda viroboti na droni.

Nchini China, kwa mfano, kampuni tano kuu za teknolojia zimejizatiti kutumia teknolojia hii kuhakikisha kuwa wanaougua hawawaambukizi wengine.

Maeneo ya Huawei, Alibaba, Baidu, Tencent na Didi kwa sasa yamekumbatia matumizi ya AI na intaneti kuwahamasisha wasiougua jinsi ya kujiepusha na maradhi hayo.

Roboti zinatumwa kuwafundisha jinsi ya kusalia salama huku droni nazo zikitumwa kuwapelekea wanaogua dawa.

Hii inapunguza mtagusano wa watu, na hivyo, idadi ya watu wanaoambukizwa imepungua wiki hii.

Pia, roboti zinatumika kusharizia dawa vyumba ambavyo vinakisiwa kuwa na virusi hivyo, huku droni zikitumwa kuwapa chakula na maji watu waliotengwa katika makazi maalum, ili wasieneze ugonjwa huo.

Mjini Seattle, Amerika, roboti imewasaidia madaktari kumtibu mwanamume aliyekuwa akiugua ugonjwa huo, kwa kufanikisha mawasiliano baina ya mgonjwa huyo na wao.

Inahakikisha tabibu hamkaribii mgonjwa, na hivyo wagonjwa wengi wanaweza kutibiwa bila ya madaktari kuhatarisha afya yao kwa kumkaribia mgonjwa.

Mjini Wuhan, ambapo ndipo asili ya virusi vya corona, magari ya kujiendesha sasa yanatumika kutuma dawa kwa wauguzi na wagonjwa, na kuwaeleza jinsi ya kuzitumia kupitia kwa sauti iliyorekodiwa.

Mbali na hayo, AI inatumika kufuatilia maambukizi kwa kunasa data ya wanaopona na wanaoangamia, na maeneo mapya ambapo ugonjwa huo unachipuka, na kuwapa wakazi taarifa na ilani kuhusu maambukizi hayo.

Hii inafaa kuwa funzo kwa Kenya, maanake nimeiona Wizara ya Afya ikitapatapa isijua ianzie wapi. Imewaambia Wakenya kuwa imetayarisha vitanda na maeneo ya kutenga watu, lakini hiyo si suluhu tosha.

Sawa na mataifa mengine yanayoendelea, Kenya inajivunia ubunifu wa kiteknolojia. Hivyo, serikali inafaa kuagiza droni na roboti hizi kutoka ng’ambo iwapo inachukulia suala hili la corona kwa uzito.

Iweje inaandaa vitanda katika hospitali ikijua fika kuwa madaktari wa serikali watalazimika kuwatibu wagonjwa kwa ukaribu, na hatimaye pia kuambukiza wataalamu ambao wanafaa kuzuia maambukizi mapya.

Watu wanaoingia nchini kutoka nje hawafai kupimwa na madaktari wakati teknolojia inaweza kufanya hivyo. Tutahadhari kabla ya hatari. Kampuni za teknolojia nchini pia zinafaa kuchangia katika suala hili.

Serikali yafaa kukomesha mapuuza haya.

Mbona ianze kuagiza vifaa hivi wakati hali ni hatari tayari na watu kadhaa kuangamia?

Siombei Kenya maradhi haya, lakini nasema kwamba tunahitaji kujiandaa vyema zaidi.