• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
NGILA: Tutumie data ipasavyo kuimarisha ukuzaji wa chakula

NGILA: Tutumie data ipasavyo kuimarisha ukuzaji wa chakula

NA FAUSTINE NGILA

CHANGAMOTO ya uharibifu wa nzige sasa ni tisho kuu kwa utoshelevu cha chakula nchini.

Nzige hawa tayari wameharibu mimea katika maeneo mengi, huku dawa za kuwauza zikijaa katika anga ya Kenya, hali ambayo inazidi kuwaua nyuki wanaotegemewa na binadamu kwa uzalishaji wa chakula.

Huku mbinu za kale zikizidi kutumiwa kukabiliana na nzige hawa, inashangaza kuwa serikali imefumbia macho mbinu za kisasa ambazo zina uwezo mkubwa wa kuwaangamiza wadudu hao.

Hii yafaa kuanza na utekelezaji wa jukwaa la kitaifa la kufuatilia data yote ya kilimo ili kuinua viwango vyetu vya ukuzaji mimea na ufugaji wa mifugo.

Kwa sasa Kenya inajivunia kuwa ya kwanza duniani kuwa na jukwaa la mitandaoni lisilo na malipo kwa watumizi, lililozinduliwa majuzi na Kituo cha Kimataifa cha Kilimo na Sayansi (CABI).

Jukwaa hili linawapa Wakenya fursa ya kupata data wanayotafuta kuhusu mimea, wadudu, magonjwa na dawa zinazofaa kwa urahisi.

Sekta yetu ya kilimo ni mojawapo ya zile ambazo zinaweza kufaidika zaidi na uchanganuzi wa kina wa data, maanake sasa huduma hii inaweza kutumiwa na kila mkulima. Ikitumiwa vizuri, itainua mavuno yao.

Hata hivyo, kuwa na jukwaa hili si suluhu tosha. Wizara ya Kilimo inapaswa kushirikiana na wakulima, maafisa wa kilimo, wataalamu na maduka ya kuuza dawa kwa uhamasisho wa uwepo wa huduma hii.

Kuzima madhara ya nzige, kwa mfano, teknolojia ya GIS ikichanganuliwa kwa undani itaweza kuonyesha nzige wanavyoenea, na kutambua dawa inayowaua bila kuua nyuki.

Kenya inahitaji suluhu za kudumu kukabili majanga haya, ambapo uchanganuzi wa data hutumika pakubwa kubashiri wadudu hatari na magonjwa yanapoingia nchini, na kubuni mikakati mwafaka ya kuyaangamiza.

Kizazi cha sasa kina bahati kuishi katika enzi za mageuzi ya kiteknolojia, ambapo baadhi ya changamoto kubwa zinatatuliwa kupitia teknolojia za kisasa.

Hata hivyo, kujikokota kwa serikali katika kutumia teknolojia hizi kunaumiza maendeleo.

Kwa kutumia teknolojia hizi pamoja na matini ya utafiti, suluhu nyingi zaweza kupatikana katika visiki vya kilimo, hasa kwa kuweka data hii mikononi mwa wale wanaoihitaji zaidi.

Tatizo kuu ni kuwa data iliyopo nchini kwa sasa haiwezi kupatikana kwa urahisi maanake imehifadhiwa katika mbinu za kale. Zinahitaji kuwekwa kwa mifumo yakidijitali.

Duniani kote, asilimia 40 ya mazao hupotea kutokana na wadudu, na tusipochukua hatua za kisasa, huenda asilimia hii ikapanda zaidi, ukizingatia madhara ya nzige.

You can share this post!

MATHEKA: Huu si wakati ufaao kwa Haji, Kinoti kuumbuana

AWINO: Mageuzi kuhusu mbolea yafaa, lakini mambo bado

adminleo