Habari

Mafundi wawili wafariki baada ya kufunikwa na mchanga Tudor

March 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

WANAUME wawili wamefariki mjini Mombasa jana Jumanne baada ya kufunikwa na mchanga walipokuwa wakitekeleza shughuli ya ujenzi.

Ajali hiyo iliyotokea mwendo wa alasiri katika nyumba za kifahari za Wonder Land, Kaa Chonjo, Tudor, ilisababisha Bw Francis Kaparo na Saidi Mlako kufariki huku wenzao wawili wakipata majeraha mabaya.

Akithibitisha mkasa huo, kamanda wa polisi kituo cha Urban mjini humo, amesema ajali hiyo ilitokea baada ya mchanga kuporomoka ghafla na kufunika watu wanne waliokuwa wakieka matuta kuuzuia.

Miili ya waliofariki ilipelekwa katika hospitali kuu ya mkoa wa Pwani Makadara huku waliojeruhiwa wakipelekwa katika hospitali ya mmiliki binafsi ya Mewa.

Kulingana na Bw Abdallah Jambia ambaye ni miongoni mwa mafundi waliokuwa katika eneo la tukio, ni kwamba takriban mafundi 20 waliingia ndani ya shimo ambalo walikuwa wamechimba na walikuwa katika harakati kulijaza mchanga huo ulipomwagika na kufunika watu wanne huku wengine wakifaulu kutoka.

“Nilikuwa nimeenda kuleta tingatinga au bora niseme mashine ya kuchota mchanga, mara nikasikia usiyahi na kufika nikaambiwa kuna watu waliofunikwa na mchanga na walihitaji kutolewa,” akasema Bw Abdallah.

Alieleza kuwa alitumia tingatinga hilo kuuondoa mchanga ili kuwanusuru waliofunikwa.

Hata hivyo, alieleza kuwa waliwapata wawili wakiwa wamefariki huku wengine wawili wakiwa katika hali mahututi.

Biwi la simanzi lilitandana sehemu hiyo huku mafundi waliyonusurika wakijilaumu kwa kushindwa kuwaokoa wenzao.