HabariSiasa

Wabunge wa Uhuru, Raila waanza kampeni ya kumng'oa Ruto

March 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

ZAIDI ya wabunge 70 wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Jumatano walianza kampeni ya kumwondoa madarakani Naibu Rais William Ruto.

Wanasiasa hao kutoka Bunge la Kitaifa na Seneti, walisema wakati umefika wa Dkt Ruto kuondoka serikalini wakidai ameshindwa kufanya kazi pamoja na Rais.

Hii imetokea siku chache baada ya Seneta James Orengo wa Siaya kufichua wiki iliyopita kuwa kuna mpango wa kuwasilisha mswada bungeni wa kumtimua Dkt Ruto.

Kulingana na Kipengele 150 cha Katiba, Naibu Rais anaweza kuondolewa afisini kwa matatizo ya kimwili ama kiakili, kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Vile vile, anaweza kuondolewa kwa kukiuka kanuni ambazo anapaswa kuzingatia kikatiba ama panapokuwepo na sababu za kutosha kuthibitisha kwamba amefanya makosa yanayokiuka sheria za kitaifa ama kimataifa, au utovu wa nidhamu kwa kukiuka kanuni anazopaswa kuzingatia kama afisa wa serikali.

Wakiwahutubia wanahabari jana, wanasiasa hao kutoka vyama vya Jubilee, ODM, Kanu, ANC na Wiper kati ya vingine, walisema kuwa kwa kuendelea kumkosoa Rais Kenyatta, Dkt Ruto anakiuka kiapo alichokula kumtii.

“Ikiwa mtu ameshindwa kufanya kazi ya mkubwa wake, basi anapaswa kujiuzulu. Ni makosa kuendelea kumshambulia mkubwa wako na taasisi zilizo katika serikali unayohudumu. Tunamwambia Dkt Ruto aondoke ikiwa imekuwa vigumu kufanya kazi pamoja na Rais Kenyatta,” akasema Mbunge wa Kieni Kanini Kega.

Pia walimlaumu kwa kutounga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao unaendeshwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Kauli zao zinajiri baada ya Dkt Ruto kudai kwamba kuna maafisa wakuu wa serikali ambao wanaendesha njama ya kuzima ndoto yake ya kuwania urais 2022.

Lakini jana, Dkt Ruto alikosolewa vikali kwa kuwaingilia maafisa ambao anapaswa kuwatetea, ikizingatiwa wako chini yake kimamlaka.

“Ni kinaya kwa Dkt Ruto kuwakosoa na kutilia shaka uwezo wa maafisa ambao wanahudumu katika serikali moja naye. Huu ni sawa na usaliti, hasa dhidi ya Rais Kenyatta,” akasema mbunge wa Kathiari Robert Mbui.

Wabunge hao walimtaja Dkt Ruto kama kiongozi asiyefaa wakisema amedaiwa kuhusika katika sakata kadhaa za ufisadi, baadhi zikiwa uuzaji wa mahindi, kandarasi tata za mabwawa ya Arror na Kimwarer, ujenzi wa hoteli ya Weston kati ya zingine.

“Vitendo hivyo vimemfanya Dkt Ruto kutofaa kama kiongozi. Kwake, kinachofaa ni kutawala Wakenya, badala ya kuwahudumia,” akasema Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Baringo Gladys Cheruiyot.