Habari Mseto

Wakuu serikalini walaumiwa kwa mauaji nchini

March 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

KIMYA cha viongozi wakuu serikalini kuhusu mauaji ya kiholela na mateso ya raia mikononi mwa maafisa wa usalama kimeonekana kukera Serikali ya Amerika.

Serikali hiyo ya Rais Donald Trump imelaumu wakuu wa wizara zinazosimamia idara za polisi, ujasusi na jeshi nchini Kenya kwa ukiukaji wa haki za binadamu unaotekelezwa na maafisa kwa raia.

Ripoti ya haki za binadamu kimataifa iliyotolewa jana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Amerika, Bw Mike Pompeo, ilibainisha serikali haikupiga hatua kulinda raia dhidi ya maafisa katili mwaka wa 2019.

Amerika ililaumu wakuu ambao si maafisa wa polisi wala wanajeshi kwa kutowajibika kudhibiti asasi zilizo chini yao ili kuzuia maafisa kutesa au kuua raia kiholela.

Ilieleza kwamba, Idara ya Polisi wa Taifa ina majukumu ya kudhibiti usalama ndani ya nchi ikiwa chini ya Wizara ya Usalama wa Nchi. Wizara hiyo inasimamiwa na Dkt Fred Matiang’i.

Iliendelea kusema, Idara ya Ujasusi Kitaifa ina jukumu la kukusanya habari za kijasusi ndani na nje ya nchi, ikiwa chini ya Rais Uhuru Kenyatta.

Kwa upande mwingine, ripoti hiyo ilisema jukumu la usalama nje ya nchi limo mikononi mwa Jeshi la Taifa (KDF) ambalo hufanya pia kazi ndani ya nchi ikiwemo kulinda mipaka, chini ya Wizara ya Ulinzi.

Wizara hiyo ilisimamiwa na Bi Raychelle Omamo hadi mwaka huu alipohamishwa kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, na nafasi yake ikachukuliwa na Bi Monica Juma.

“Wakati mwingine, wakuu ambao ni raia wasio polisi wala wanajeshi hawakudhibiti vikosi vya usalama ipasavyo,” sehemu ya ripoti hiyo inayojumuisha masuala ya haki za binadamu katika mataifa 199 inasema.

Matokeo yake ni kwamba, visa vya ukiukaji wa haki za raia vilishuhudiwa sana ikiwemo mauaji ya kiholela yaliyotekelezwa na maafisa au magaidi, wananchi kutoweka baada ya kukamatwa na polisi, mateso ya raia mikononi mwa maafisa wa usalama miongoni mwa visa vingine vingi.

Bw Pompeo alisema lengo la Amerika kutoa ripoti aina hiyo kila mwaka ni kukumbusha kila serikali kuwa ni sharti watimize haki za binadamu.