Makala

KIKOLEZO: Usimwone Papa Mokonzi hivyo, visanga vyake ni vingi

March 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na THOMAS MATIKO

KWA mzee mwenye umri mkubwa wa miaka 63, utakachotarajia kutoka kwake ni wingi wa busara tu.

Busara ya kukaa na watu wa aina aina, kimaarifa na upevu wa maisha, upole na ukomavu.

Lakini pengine hizi ni kati ya sifa ambazo hutazipata kwake Le Grand Mopao, Papa Mokonzi, Antoine Koffi Olomide.

Katika maisha yake kafanikiwa pakubwa. Kama ni pesa anazo. Umaarufu ndio usiseme. Ushawishi nao, acha kabisa.

Alianza kutengeneza noti tangu miaka ile ya ‘90, kama ni kujichanganya na watu maarufu kuanzia wafalme, Marais, wajasiriamali watajika na watu wengine wa tabaka hilo, imekuwa kitu cha kawaida sana kwake.

Koffi Olomide ameibuka kuwa mmoja wa wanamuziki wakubwa duniani tangu akiwa kijana na mpaka sasa uzee ukiwa umemkamata. Anapendwa na wengi kutokana na uwezo wake wa kutoa ‘hit’ baada ya nyingine pamoja na uwezo wake mkubwa wa kutoa burudani ya kishua kwenye shoo za laivu.

Licha ya kusifiwa kwa kila hali, Koffi katokea kuwa na upungufu mbaya wa kitabia. Ni upungufu ambao umekuwa ukilitia doa jina lake. Upungufu wa kuchemkwa na hasira za haraka zinazoambatana na kiburi na ujeuri.

Tabia hizo zimemponda mara si moja, na ndio zilizopelekea yeye kupigwa marufuku kuingia nchini miaka minne iliyopita baada ya kumvunja mmoja wa madansa wake kwa kumpiga teke katika uwanja wa ndege wa JKIA.

Wiki hii aliingia nchini kimya kimya baada ya serikali kumwondolea marufuku ile. Alikuwa ni mpole ajabu. Aliomba msamaha kwa mara ya mia na, kwa kitendo kile. Lakini ni vigumu sana kumzungumiza Koffi bila skendo zake kukujia akilini. Kama hizi:

ACHANA PASPOTI ZA WAPAMBE WAKE

Kwa hasira zake hizo, Koffi aliwahi kuchanachana paspoti ya mmoja wa madansa wake. Hii ilikuwa ni katika miaka ya 90 hivi na cha kushangaza ni kuwa tukio hilo lilitokea humu nchini Kenya. Koffi aliripotiwa kufanya uharibifu huo kwa madai kuwa dansa huyo alikuwa akimchafulia jina, japo haijawahi kubainika kivipi.

Lakini hiyo haikuwa mara ya kwanza kumsababishia mpambe wake hasara ya namna hiyo. Mnamo 1998 kwenye ziara yake nyingine nchini, Koffi alichanachana pasipoti pia ya mmoja wa wanamuziki wake Suzuki Luzubu aliyekuwa katika bendi yake ya Quartier Latin International aliyoianzisha 1986.

MADAI YA UBAKAJI

Ufaransa ameanza kuishi juzi baada ya kufungiwa kuishi kule kwa miaka 10 kutokana na kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili. Tangu 2012 alikuwa na kesi iliyomalizika yapata mwaka mmoja uliopita. Alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kuwabaka madansa wake alipokuwa nchini humo kwa ajili ya shoo. Aliposhtakiwa, Koffi aliamua kutoroka Ufaransa anakoishi mamake, ili kukwepa kujibu mashtaka hayo. Baada ya shtuma hizo, Koffi alidai kuwa madansa hao walitaka tu kumchafulia jina kwa lengo la kusaka fedha kutoka kwake.

NCHI NYINGI ZAMKATAA

Ukiachana na Kenya, Koffi amewahi kukataliwa katika mataifa mengine kutokana na tabia zake hizo chwara.

Ufaransa iliwahi kumpiga marufuku 2012 baada yake kuamua kukwepa kesi ya ubakaji ya madansa wake.

Nchini Zambia japo bado hajafungiwa kuzuru, pia wameonyesha kukerwa na tabia zake ambapo 2013 anadaiwa kumtandika kofi nzito mpiga picha mmoja kwa kumuuliza maswali ya kibinafsi.

MPENDA VITA

Kando na kumtandika teke dansa wake JKIA Julai 2016, na vilevile kumzaba kofi mpiga picha kule Zambia, Koffi amewahi kuhusika na visanga vingine vya kivita. Agosti 2012 aliwahi kushtakiwa kwa kumtandika na kumuumiza produsa wake mmoja katika hoteli moja ya kifahari kule kwao Kinshasa kutokana na mzozo wa Euro 3,000 (Sh335,000).

Akiwa nchini Zambia Januari 2013 kipindi alichomzaba kofi mpiga picha, alitekeleza unyama huo tena kwa dansa wake baada ya shoo.

AJIBATIZA JINA ‘PAPA MTAKATIFU’

Koffi amekuwa na tabia ya kujibandikia majina ya utani akiwa na zaidi ya 35 . Lakini kuna kipindi alivuka mipaka na kuamua kujibatiza jina la Papa Mtakatifu ambaye ni kiongozi wa kanisa la Katoliki duniani.

Ishu hiyo ilizua balaa mjini Kinshasa huku kanisa la Katoliki likiamua kumwandama alipoamua kujipa jina la papa mtakatifu ‘Benedict XVI wa Congo’.

Na kama haitoshi, alikwenda zaidi na kuchapisha mabango yenye jina hilo na kutundika katika miji yote mikuu ya Kinshasa. Ni jambo lililochukuliwa kuwa la dharau na la kumdhalilisha Papa Benedict XVI aliyejiuzulu wadhifa huo kutokana na kusumbuliwa na maradhi.

AONYESHA UJEURI CAMEROON

Wakati wa mojawapo ya ziara zake nchini Cameroon 1991, Koffi aliripotiwa kuchukizwa na jinsi alivyopokelewa nchini humo na kuapa hatawahi tena kukanyaga katika taifa hilo.

Mojawapo ya vitu vinavyosemekana kumchukiza ni pale alipopokelewa kwa gari la kifahari la ‘Limousine’ ambalo alikataa kuliabiri kwa sababu halikuwa na kiyoyozi (Air Conditioner).