• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Mung’aro aahidi Wapwani hatimiliki

Mung’aro aahidi Wapwani hatimiliki

Na CHARLES LWANGA

WAZIRI msaidizi wa Ardhi, Bw Gideon Mung’aro amesema serikali inapanga kutoa hatimiliki za ardhi 8,000 katika Kaunti ya Kilifi mwaka 2020 katika hatua ya kukabiliana na tatizo la uskwota eneo hilo.

Bw Mung’aro alisema Wizara ya Ardhi ikishirikiana na Tume Huru ya Ardhi (NLC) zinataka kutatua mizozo ya ardhi eneo hilo ambayo imegeuza maelfu ya wakazi kuwa maskwota.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi baada ya kuhudhuria ibada ya mchango wa kanisa, Bw Mung’aro alisema nia yao ni kutetea haki ya wakazi ya kumiliki ardhi baada ya kupokea ripoti kuwa baadhi ya mabwanyenye wamenyakuwa ardhi yao.

“Tume ya NLC tayari imeanza kuchunguza madai ya unyakuzi wa mashamba baada ya mabwanyenye kujitokeza na kudai umiliki wa ardhi ambazo wakazi wamekuwa wakiishi kwa miaka na mikaka, tangu enzi za mababu zao,” alisema.

Bw Mung’aro alisema kwamba wangali wanasubiri ripoti kutoka kwa NLC ili waishughulikie na kutatua shida hiyo.

“Pia tunachunguza ripoti za kuwepo mabwanyenye ambao wanadai kumiliki ardhi na hawajawahi kuonekana, kisha hujitokeza na kulalamika kuwa maskwota wamevamia ardhi zao,” alisema na kuongeza: “Baadhi yao huleta nakala ya cheti cha umiliki ardhi badala ya cheti chenyewe ambacho wakati mwingine huwa ghushi.”

Bw Mung’aro alisema kuwa sheria inasema wazi kuwa wakati wa urithi, mtu anafaa kupeleka cheti ili apewe cheti cha umiliki mpya lakini baadhi ya wakazi hawazingatii sheria hii na bado wangali na vyeti vya umiliki vya zamani.

“Tumejadiliana na wizara husika na kukubaliana kuwa kutakuwa na majadiliano kabla ya kutimiza amri ya kufurusha maskwota,” alisema.

Rangi

Kwingineko mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amemtaka Gavana wa Kilifi Amason Kingi atoe amri itakayowalazimu wanabiashara mjini Malindi wapake majumba yao rangi.

Alisema hatua hiyo itawezesha majumba ya zamani yaliyochakaa ndani ya mji huo wa kitalii kupendeza machoni ili kuvutia watalii wa ng’ambo na humu nchini.

Akizungumza katika uwanja wa Alaskan mjini Malindi katika mkutano wa kuzindua miradi wa maendeleo ya Gavana Kingi, Bi Jumwa alisema ingawa gavana amewekeza pesa nyingi katika miradi ya maendeleo mjini humo, ili kuvutia watalii, upakaji majumba rangi utavutia watalii wengi mjini humo.

“Malindi ni mji ambao umesifika sana kutokana na utalii na unajulikana kama Milan ndogo kwa sababu unapendwa sana na Waitaliano lakini majumba mengine mjini yameparara na yanatisha kutokana na uzee. Namwomba gavana atoe amri yapakwe rangi ili yapendeze na kuvutia watalii,” alisema.

Bi Jumwa alisema kuwa yeye hukerwa na majumba machafu yaliyochakaa kila mara anapozunguka mjini Malindi na ana matumaini kuwa Gavana Kingi ataitikia ombi lake litakalowezesha mji huo kuvutia zaidi.

You can share this post!

Hamning’oi kitini, Ruto ajibu wabaya wake

DAU LA MAISHA: Anahamasisha mtoto wa kike kusomea sayansi

adminleo