Habari Mseto

Refarenda itafungua safari ya Odinga kuingia Ikulu – Wandayi

March 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DICKENS WASONGA

CHAMA cha ODM kitaanza kampeni ya kuhakikisha kiongozi wake Raila Odinga atashinda urais baada ya kura ya maamuzi inayotarajiwa, mkurugenzi wa masuala ya kisiasa wa chama hicho, Opiyo Wandayi, amesema.

Matamshi ya mbunge huyo wa Ugunja ni miongoni mwa vidokezo vya wandani wa Bw Odinga kwamba atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kiongozi wa wachache katika seneti ambaye ni seneta wa Siaya James Orengo, amekuwa akimhimiza Bw Odinga kugombea urais kwa mara ya tano.

Ingawa amekuwa akisema kuwa muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta sio kuhusu uchaguzi wa 2022, Bw Odinga amekuwa akiwakumbusha wafuasi wake kwamba Mpango wa maridhiano (BBI) utawawezesha kuingia Canaan.

Wiki moja lililopita, aliwaambia waombolezaji katika mazishi ya Profesa Gilbert Ogutu huku Bondo, kwamba mamba waliomzuia kufika Canaan wameondolewa na Rais Kenyatta kupitia handisheki yao.

Bw Wandayi alisema kwamba chama cha ODM kina mikakati ya kuhakikisha kitaunda serikali ijayo na kuhakikisha ni watu wanaofaa watakaotekeleza mchakato wa BBI.

Alisema Bw Odinga atatekeleza wajibu mkubwa katika serikali ijayo na kuongeza kuwa chama hicho kitazindua kampeni yake ya kuelekea uchaguzi wa 2022 baada ya kura ya maamuzi.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa Kenya itafanya refarenda kabla ya mwisho wa Julai 2020.

Akizungumza akiwa eneobunge lake alipofungua ofisi ya naibu kamishna, Bw Wandayi alisema kwamba chama cha ODM hakitamruhusu naibu rais William Ruto kuongoza nchi hii 2022 akisema hatatekeleza mageuzi ya kikatiba.

“Hatuwezi kung’ang’ana kuwa na katiba mpya na kisha tuiache katika mikono ya watu wasioweza kuitekeleza,” alisema.

“Kuna mambo makubwa tunayomezea mate kama chama. Punde tu baada ya kumaliza kura ya maamuzi, hatutapumzika, tutaanza safari ya kuelekea 2022,” alifichua.

Kulingana na mbunge huyo, Jopokazi la Maridhiano limekusanya maoni mengi ya kuiwezesha kuandaa refarenda na kwa hivyo marufuku ya mikutano ya BBI haitaathiri mchakato huo.

“Wakenya wamezungumza. Wametoa maoni yao katika mikutano ya hadhara iliyofanyika maeneo tofauti nchini. Wengine wamewasilisha memoranda na hii inatosha kubadilisha katiba,” aliongeza.

Alisema nchi haina wakati wa kupoteza na ni lazima kura ya maamuzi ifanyike Julai. Bw Wandayi alidokeza kuwa ODM kitaendelea kumtetea Rais Kenyatta dhidi ya mashambulio ya wanasiasa wa kundi la Tangatanga linalomuunga mkono Dkt Ruto.

“Hatuna shida na Ruto binafsi lakini akithubutu kumshambulia rais au Bw Odinga, tutakabiliana naye,” alisema.

Aliendelea kufichua kuwa ODM kitawakaribisha wanachama wote waliokihama mwaka wa 2017 na kwamba kila mmoja ana haki ya kugombea wadhifa wowote uchaguzi wa chama utakapoitishwa.

“Tunataka kila mtu kuwa nasi wakiwemo wenzetu waliokuwa wagombeaji huru wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ili kutia chama nguvu,” alisema.