KINAYA: Jubilee si lolote si chochote
Na DOUGLAS MUTUA
CHAMA cha kuku, ama ukipenda Kanu, kilikipata!
Kabisa, kilipothubutu kumeza tingatinga na moshi wake.
Kilivimbiwa kikalazimika kutapika, kikabaki hoi, mpaka sasa kinatapatapa. Kinaona vimulimuli, mazingaombwe, kina kisunzi tele.
Hata wewe, ikiwa una akili razini, ungawa jogoo unawezaje kumeza tingatinga linalobomoa nyika na kuifanya shamba?
Nashukuru Maulana kwa kuniweka hai nishuhudie historia ikijirudia. Tusidanganyane: Jubilee imekwisha! Hamna kitu.
Mwana wa Jaramogi, sawa tu na alivyomhangaisha mwendazake Mzee Kirungu na chama chake cha kuku, ameichanachana Jubilee kama tambara la mwendawazimu!
Ama unataka kuniambia hujakutana na wanasiasa wa Jubilee wakirusha mikono hewani na kujizungumzia mambo yasiyoeleweka? Wanauliza ‘kwani kuliendaje?’
Tangu hapo nikiambiwa kila soko lina mwendawazimu wake, lakini sikutahadharishwa kwamba soko moja linaweza kuwa na wendawazimu wengi kuliko watu timamu.
Nakataa kuwa muovu kama baadhi ya Wakenya wenye hasira ambao nimewaona mitandaoni wakiomba upepo wa Coronavirus upitie bungeni kuwaadhibu wakora fulani.
Nakataa kuwa muovu kama wengine waliotia dua ya kuku dhidi ya mwewe, eti nzige waliotua nchini wafike bungeni na kuingia machoni mwa wakora hao.
Nataka wakora wetu wawe salama hadi hapo 2022 ambapo nakuhakikishia takriban asilimia 75 watatemwa na wananchi kama kikohozi cha Coronavirus.
Hatukuwachagua wakahasimiane, kutishiana wala kututumuliana misuli kana kwamba wanajiandalia michezo ya olimpiki. Kazi yetu hawafanyi, wanajaza matumbo yao.
Mara hii nakataa kumlaumu Agwambo. Nitampongeza kwa kuwa mjanja. Alipojinyima, bila kujua, fursa ya kuingia bungeni akishindwa uchaguzi wa urais alizua mbinu nyingine.
Katiba ya 2010, ambayo aliivumisha kuliko BBI, ilihakikisha kwamba akishindwa kikweli au kura zake ziibwe angekaa nje ya Bunge.
Hivyo ilibidi atafute njia ya kujidumishia ushawishi wa kisiasa. Hebu mvulie kofia kwa kuwatoa wabunge bungeni waje huku nje wampiganie badala yake yeye kuwafuata huko.
Ni watu wangapi nchini Kenya walio na uwezo huo? Aliketi nje ya Bunge kati ya 2013 na 2017, wengi wakamcheka eti hana kazi, kumbe Mungu wake halali!
Dua yake ilijibiwa, yule mjanja mwenyeji wa Ikulu akawa amepanga wakati murua wa kumtumia Agwambo.
Tulikutabiria hapa, tukakwambia mchuuzi kuku wa Sugoi alikuwa msindikizaji watu, kwamba angetupwa nje baada ya uchaguzi mkuu uliopita, lakini hukutusikiza.
Ndivyo siasa zilivyo kote duniani; ukiitumia ngazi kukwea, jukumu lako la kwanza ni kuiangusha au kuivunjavunja asitumie mwingine kukufikia.
Hivyo ndivyo Jubilee inakufa kifo cha kasi mikononi mwa Agwambo, tena kwa raha za mwana wa Jomo.
Changamoto yangu kwa Agwambo mara hii ni kwamba awe mwanamume kamili, afike Ikulu alikotamani kufika miaka yote hii, asiwe kama kiko ambacho hutumiwa kupakua mchuzi na wala hakili.
Ni changamoto kwani najua mwana wa Jomo hajaacha janja zake, angali anatafuta njia ya kumwangamiza Agwambo kisiasa akishamsaidia kumzima mchuuzi wa Sugoi.
Ikiwa Agwambo ataruka mtego huo, hapo ndipo nitakubali yeye ni mwanamume kamili. Tangu hapo sijapenda kisingizio chake kwamba kura zake zinaibwa.
Nina ugumu wa kumpa mtu kura yangu ikiwa hawezi kuitunza. Wanaume ni kuonana, twende nalo!