• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 9:58 AM
SHINA LA UHAI: Ongezeko la mimba za mapema fumbo linalotatiza wataalamu

SHINA LA UHAI: Ongezeko la mimba za mapema fumbo linalotatiza wataalamu

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA umri wa miaka 16 pekee, Tsuma, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika kijiji cha Maweni, Kaunti ya Kilifi analazimika kusawazisha kati ya kuwa mwanafunzi na kuwa mama.

Sharti ajitahidi kusoma huku akimshughulikia mwanawe wa mwaka mmoja unusu, suala ambalo limekuwa changamoto ambayo imewalazimu baadhi ya wasichana wenzake kutoka kijijini mwake kusahau kabisa ndoto ya kuendelea na masomo.

Tsuma ndiye msichana wa kipekee kurejea shuleni baada ya kujifungua, miongoni mwa wengine 15 katika kijiji chake, walioshika mimba wakiwa wangali shuleni.

Alipogundua kwamba alikuwa mjamzito, aliendelea na masomo hadi alipofika miezi minane ambapo alisalia nyumbani hadi alipojifungua.

“Kisha nilirejea shuleni mtoto alipotimu miezi sita,” aeleza.

Uamuzi wake wa kurejea shuleni umemfanya kuheshimiwa kijijini mwake, lakini bado anakumbwa na changamoto inayotokana na kuwa mama mchanga, na wakati huo huo mwanafunzi.

Kwa mfano, analazimika kulipa nauli ya Sh100 ya usafiri wa boda boda kila siku kwenda shuleni na kurejea nyumbani, mzigo mkubwa hasa ikizingatiwa kwamba yeye ni yatima, na shangaziye anayeishi naye na ambaye ni mchuuzi wa mboga, hawezi kumudu gharama hizi.

Kwake Sheila, kutoka eneo la Mtwapa Posta, kila siku ni mahangaiko katika jitihada za kumtafutia lishe mwanawe wa miaka miwili.

Katika kipindi cha miaka miwili, Sheila ambaye kwa sasa ana miaka 22 amelazimika kuchukua hatamu na kutimiza majukumu ya kuwa mama na baba kwa mwanawe.

Hadithi yake inafanana na yake Catherine, aliyemzaa bintiye miaka miwili iliyopita, wakati huo akiwa na miaka 21 pekee.

Huku akiwa na elimu duni na kutokana na sababu kuwa anatoka katika familia maskini, amelazimika kufanya kazi za sulubu ili kukidhi mahitaji ya mwanawe.

Tsuma, Sheila na Catherine wanaakisi changamoto zinazowakumba wasichana wanaojifungua wakiwa wangali wachanga kiumri, kabla ya hata kukamilisha masomo.

Utafiti uliofanywa na Hazina ya Umoja wa Mataifa inayohusika na idadi ya watu UNFPA ilionyesha kwamba kati ya Juni 2016 na Julai 2017, wasichana 378,397 katika umri wa miaka 10 na 19 nchini Kenya, walishika mimba.

Aidha, visa vya ujauzito, vile vile idadi ya wasichana wanaopata watoto katika umri wa kubaleghe nchini Kenya ni asilimia 18, huku tafiti zikiashiria kwamba mmoja kati ya wasichana watano katika umri wa kubaleghe amewahi kujifungua mtoto aliye hai au amebeba mimba yake ya kwanza.

Katika Kaunti ya Kilifi, uhalisi wa janga la mimba za mapema miongoni mwa wasichana wadogo linahisiwa katika kituo cha kiafya cha Mtwapa kinachoshughulikia akina mama wachanga.

Bi Violet Muinde, afisa wa afya na msimamizi wa mradi wa kituo cha kimataifa cha afya ya uzazi (ICRHK) katika kituo hiki anasema kwamba kumekuwa na ongezeko la visa vya mimba miongoni mwa wasichana wadogo, suala linalotisha.

Kituo hiki ambacho kimekuwa kikitoa huduma za mpango wa uzazi, usaidizi wa kisaikolojia, vile vile usaidizi wa bidhaa kwa akina mama wachanga, kimeshuhudia ongezeko la idadi ya akina mama wachanga wanaozuru hapa wakitaka usaidizi.

“Tangu nilipoanza kuhudumu katika kituo hiki, tumeshughulikia zaidi ya wasichana 2,000,” aeleza.

Basi tatizo ni nini?

Baadhi ya mambo yanayochochea mimba za mapema miongoni mwa wasichana wadogo ni ukosefu wa usawa wa kijinsia, ndoa za mapema, umaskini, dhuluma za kijinsia, ukosefu wa masomo na nafasi duni za kazi.

Bi Flora Chari Ali, mkufunzi wa masuala ya kijamii na mwanaharakati wa haki za kibanadamu eneo la pwani anasema kwamba vijana wanazidi kujihusisha na masuala ya ngono katika umri wa chini.

“Mtindo wa kisasa wa maisha pia umechangia tatizo hili. Idadi ya vijana wanaotumia kinga wanapojihusisha na ngono ni ndogo sana, suala ambalo mbali na kuwaweka katika hatari ya kushika mimba za mapema, linawaweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa na hasa virusi vya HIV,” aongeza.

Mwaka jana, Waziri wa Elimu Prof George Magoha aliwaelekezea wazazi kidole cha lawama ambapo aliwalaumu kwa kutelekeza majukumu yao ya kuwazungumzia watoto wao kuhusiana na masuala ya ngono na hatari zinazohusishwa na kushiriki tendo la ndoa mapema.

“Mimba za mapema zinasababisha wanafunzi kuacha shule, na hivyo lazima wazazi wawajibike vilivyo na kuwashauri watoto wao kila wakati,” alisema. Kwa upande mwingine, Bi Ali anasema japo mtindo wa kisasa ni kichochezi, umaskini pia umechangia pakubwa tatizo hili.

“Kutokana na matatizo ya kiuchumi wasichana wengi wanaoishi katika sehemu zinazokumbwa na umaskini kama vile Kilifi, wanajihusisha na tendo la ndoa kama mbinu ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Kwa mfano, kwa sababu ya umaskini, wasichana wengi wanalazimika kutembea kwa mwendo mrefu kwenda shuleni na kurejea nyumbani, suala linalowafanya kuwa windo rahisi la wanaume,” aeleza.

Kulingana na Bi Ali, pia ni wakati wa kukiri kwamba suala la akina mama wachanga limechangiwa na visa vya unajisi.

Ripoti iliyochapishwa na shirika la Afya ya Uzazi, International Center for Reproductive Health, mwaka wa 2012 ilionyesha kwamba asilimia 80 ya waathiriwa wa unajisi kwa kawaida huwa wanawake, huku wengi wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Kulingana na Bi Sabia Mwinyi, mhudumu anayesimamia kitengo cha kuhudumia waathiriwa wa dhuluma za kimapenzi na kijinsia katika Hospitali Kuu ya Pwani (Coast General Hospital), kwa upande mwingine watekelezaji unyama huu huwa kati ya miaka 20 na 40.

Haya yakijiri, ni mzigo upi wa kiafya unaosababishwa na ongezeko la visa hivi?

Tafiti kadhaa zinaonyesha kwamba, takriban mmoja kati ya wasichana watano katika umri wa kubaleghe nchini ana mtoto, suala linaloweka mzigo mkubwa katika sekta ya afya nchini.

Kwa mfano, matatizo yanayotokana na ujauzito yanaorodheshwa ya pili kwa kusisababisha vifo miongoni mwa wasichana kati ya miaka 15 na 19.

Aidha, watoto wanaozaliwa na akina mama wachanga wako katika hatari ya kukumbwa na matatizo ya kukua kimwili na kiakili.

Shirika la Utafiti wa Watu na masuala ya Kiafya nchini, Kenya Demographic and Health Survey, lilifanya utafiti 2014 na kupata kuwa wasichana ambao wamekamilisha shule ya upili kwa kawaida wanapata watoto watatu maishani mwao, wakilinganishwa na wasichana ambao hawajakamilisha shule wanaozaa hadi watoto sita.

Aidha, takriban asilimia 60 ya wasichana ambao wamekamilisha shule ya msingi na upili wanatumia mbinu za upangaji uzazi, wakilinganishwa na asilimia 15 ya wale wasio na elimu.

Anasema kwamba, jamii ina jukumu la kukomesha visa hivi. “Wale wanaowadunga mimba wasichana wadogo wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya unajisi.

Kulingana na Muinde, mara nyingi, shughuli za uhamasishaji kuhusu hatari za kujihusisha na ngono mapema huelekezwa tu wasichana.

“Mafunzo haya pia yanapaswa kuwahusisha pia wavulana na wanaume,” anasema.

Anasema kwa kutoa elimu ya kina kuhusiana na suala hili, kutoa huduma za kupanga uzazi zinazowafaa vijana, watahakikisha kwamba wasichana wanapanga maisha yao na kufanya uamuzi wenye busara maishani.

Kwa upande mwingine, Flora anasema kwamba jamii inapaswa kuhamasishwa vilivyo ili watu wawe na uwezo wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaowatunga wasichana wadogo mimba.

“Serikali pia inapaswa kusimama kidete na kuhakikisha kwamba wahusika wanaadhibiwa.”

You can share this post!

Corona yaua kocha

SHINA LA UHAI: Ndimu kutibu COVID-19 ni ‘Fake...

adminleo