Wakazi Samburu walia hakuna maji corona ikienea
Na GEOFFREY ONDIEKI
Hali ya wasiwasi imetanda katika kaunti ya Samburu kufuatia ukosefu wa maji ikizingatiwa virusi vya corona sasa vinaenea.
Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali umebaini kuwa idara muhimu zimekumbwa na ukosefu wa maji kwa mwezi mmoja iliyopita.
Tatizo la ukosefu wa maji limekumba miji kadhaa ikiwemo Maralal,Wamba na Achers Post.
Wakazi waliojawa na ghadhabu wameeleza kupata wakati mgumu kufanya shughuli za kila siku ikiwemo biashara.
Wakazi hawa pia wanahofia kuzuka kwa magonjwa mengine ya maji kama vile kipindupindu.
Amos Lewarani ambaye ni mkazi wa mji wa Maralal alisema kuwa kuwa wanaishi kwa hofu ya kupata magonjwa yanayotokana na maji kwa sababu wanatumia maji ambayo hayajatiwa dawa. Pia, Taifa Leo umebaini kuwa maji ya chumvi yanayouzwa kwa bei ghali yamekuwa adimu.
“Tonahofia kupata kipindupindu kwa sababu maji yanayouzwa hapa na madalali hayajatiwa dawa,” Bw Lewarani aliambia Taifa Leo.
Uhaba huo wa maji umelemaza shughuli muhimu ya kunawa mikono kufuatia tishio la virusi vya Corona. Sehemu ambazo zimeathiriwa ni pamoja na mikahawa, baa na vituo vya afya, hivyo kulazimu wakazi kununua bidhaa hiyo muhimu kwa bei ghali.
Mkazi mwingine, Eunice Nasiaku alishutumu kampuni ya usambazaji maji katika kaunti ya Samburu (Sawasco) kwa kushindwa kusuluhisha matatizo ya maji hata baada ya kupewa malilio kwa mwezi mmoja iliyopita.
“Wanatuhubiria tuwe tukinawa mikono tusiambukizwe na virusi vya Corona. Wanataka tutumie mate yetu kunawa mikono? Hawako makini na kazi,” Bi Nasiaku aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya moja kwa moja.
Mtungi mmoja wa maji ya chumvi unauzwa takriban shilingi hamsini.
Hata hivyo afisa mkuu wa maji na mali asili wa kaunti ya Samburu Ropilo Lenyasunya alisema kuwa serikali inafanya kila juhudi kurejesha huduma kama awali.
Alisema kuwa idara yake imenunua dawa ili kutibu maji yaliyo kwenye mabwawa yote kwenye kaunti hiyo.
“Tunajaribu sana kurejesha huduma na kuhakikisha kila mkazi anapata maji kuanzia Alhamisi hii ili kuwawezesha kufanya usafi wa kunawa mikono,” alisema.