Covid-19 yayumbisha mapato uchukuzi wa umma
Na LAWRENCE ONGARO
WAWEKEZAJI na wafanyakazi katika magari ya uchukuzi wa umma mjini Thika sasa wanasema biashara imeanza kudorora.
Katibu wa Chania Sacco Bw Njenga amesema kampuni hiyo kuanzia leo Jumatano imeanza kushuhudia kudorora kwa biashara hasa wakati huu ambapo wengi hawasafiri kuepuka Covid-19.
“Baada ya ofisi nyingi za serikali kufungwa mnamo Jumanne, wafanyakazi wengi wamebaki nyumbani ambapo wasafiri ni wachache mno katika vituo. Imebidi tutumie wakati huu kupeleka katika karakana baadhi ya magari yetu,” amesema Bw Njenga.
Amesema Chania Sacco imewaajiri madereva wapatao 200 na utingo 180 huku akisema magari ambayo yanahudumu baina ya Thika na Nairobi ni kati ya 150 na 200 kwa siku.
Amezidi kusema ya kwamba iwapo hali hiyo itaendelea hivyo kwa muda wa wiki mbili hivi, kampuni yao ya Chania Sacco, itapata hasara kubwa ya zaidi ya Sh10 milioni.
“Ama kwa hakika hatungetaka jambo hilo liendelee kwa muda mrefu kwa sababu litatikisa sekta ya matatu kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Bw John Kiarie Gicharu, ambaye ndiye mwenyekiti wa Chania Sacco anasema kwa siku mbili zilizopita wameanza kuona kazi ikirudi chini jambo ambalo anasema sio mwelekeo mwema katika sekta hiyo.
“Tunajua sekta ya matatu ni kiungo muhimu nchini na kwamba mapato yakififia, basi madereva na utingo watakuwa pabaya,” amesema Bw Gicharu.
Amesema magari hayo ya matatu yalinunuliwa kwa mkopo na kwa hivyo usafiri ukikosekana bila shaka kila kitu kitasimama na madereva wengi watakosa ajira.
Ameunga mkono pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta, la kutenga siku ya Jumamosi, Machi 21, 2020, kuwa ya maombi kwa nchi ili “tuweze kujiepusha na janga hili la Covid-19.
Amesema watazidi kulipisha nauli ya kawaida ya Sh100 kutoka Thika hadi Nairobi ili wasafiri wao – wateja – wasiumie zaidi.
“Tunaelewa hali ya maisha itazidi kuwa ngumu kwa kila mmoja wetu na kwa hivyo sisi tunaotoa huduma ya usafiri ni sharti tuwe wangwana kwa kila mtu,” amesema mwenyekiti huyo.
Katika usafi, sekta ya matatu mjini Thika inaendelea kuchukua tahadhari ya kunawisha wasafiri mikono kabla ya kuabiri vyombo vya usafiri..
Chania Sacco inaongoza kampeni hiyo ambapo wakati wote wasafiri wanapoingia kwenye matatu, wanalazimika kunawa na kusafisha mikono kabla ya kuabiri matatu.
Katibu Bw Njenga amesema wako chonjo kuona ya kwamba wanapambana na Covid-19.
Mashirika mengine ya Sacco yanayofuata mkondo huo ni Super Metro, ISKA, na Chania Kibwezi.