Ofisi ya ustawishaji jiji la Nairobi yabuniwa
Na SAMMY WAWERU
MAJUKUMU muhimu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi yameelekezwa kwa ofisi mpya na maalum iliyobuniwa ili kustawisha jiji la Nairobi.
Ofisi hiyo, Nairobi Metropolitan Services (NMS) na itakayoongozwa na Meja Jenerali Mohammed Abdallah Badi, inatazamiwa kusimamia huduma za afya, uchukuzi, uimarishaji mji wa Nairobi ikiwa ni pamoja na huduma kwa umma.
Akizungumza Jumatano katika Ikulu jijini Nairobi, wakati wa utiaji saini mkataba wa kuhamisha majukumu hayo kutoka serikali ya kaunti hadi ile ya kitaifa, Rais Uhuru Keyatta ameeleza kusikitishwa kwake na hali ya jiji la Nairobi, “utupaji taka kiholela ukipaka tope sura ya nchi hii”.
Akielekeza NMS kuweka mikakati kabambe kwa muda wa siku 100 zijazo, itakavyoimarisha hali ya Nairobi, Kenyatta amesema upungufu wa maji ni suala ambalo ofisi hiyo inapaswa kuangazia ipasavyo.
Rais pia ametaja ufisadi kama donda ndugu lililoota na kukita mizizi pamoja na kutawala jumba la City Hall, ilipo ofisi ya Gavana wa Nairobi.
“Janga kuu linalogubika jiji la Nairobi hasa jumba la City Hall ni ufisadi. NMS ing’oe matapeli wote walioshika mateka jiji hili na kuzuia maendeleo na ukuaji wake,” ameagiza Rais Kenyatta.
Amesema utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara na huduma mbalimbali pia umejawa na dosari, kufuatia ufisadi unaosakatwa.
Rais pia ameagiza ofisi hiyo kuhakikisha vipande vya ardhi na ploti zote za umma zilizonyakuliwa zimerejeshwa.
“NMS iwajibikie maendeleo ya jiji la Nairobi, tunataka huduma zifikie kile mkazi na raia,” akasema.
Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa wametia sahihi uhamishaji wa huduma hizo.
Meja Jenerali Mohammed Abdallah Badi, atasaidiwa na naibu wake aliyeteuliwa, Enosh Onyango Momanyi.