Avurumishia pasta makonde hadharani
Na CORNELIUS MUTISYA
KATOLONI, MACHAKOS
Kioja kilizuka eneo hili polo aliyejawa na hasira za mkizi alipomparamia pasta na kumzaba makonde akimlaumu kwa kuvuruga mipango yake ya harusi na mwanadada muumini wa kanisa lake.
Kulingana na mdokezi, polo alianzisha urafiki na mwanadada kanisani na penzi lilipokoleza wakaamua kufunga ndoa hivyo wakapasha habari hizo jamaa zao na pasta.
“Polo aliamua kutangazia ndugu na marafiki mipango ya harusi. Walimwendea pasta wa kanisa lao ili awape baraka na kuwa kiungo muhimu katika matayarisho ya harusi yao,’’ akasema mdokezi.
Inasemekana kwamba, pasta alipopashwa habari za ndoa hiyo, alifurahia na kusema kuwa angehakikisha wawili hao wametimiza azma yao.
Aliwaalika wote wawili katika ofisi yake ili kuwapa ushauri na pia kuwaombea wapate baraka katika harusi yao. Alionekana kuunga mkono mipango ya wawili hao kikamilifu.
Hata hivyo inadaiwa siku moja pasta alimwita mwanadada huyo kwake na akamkanya dhidi ya kuolewa na polo.
Alimwambia kuwa alipata maono kuwa hakuwa mtu wa kuaminiwa na ndoa yao ingejaa kisirani.
Mwanadada huyo alishtushwa na ushauri wa pasta na akaamua kukatiza mipango ya harusi.
“Mwanadada alimwendea polo na kumwambia peupe kuwa asahau kumuoa maana hakuwa na hamu ya kuolewa,’’ alisema mdokezi.
Polo alipopata habari hizo alijawa na huzuni na akaamua kudadisi sababu ya kidosho kughairi nia ilhali mipango ya ndoa yao ilikuwa inaelekea kukamilika.
Na ukweli ukafichuka kuwa pasta kamshauri demu asiolewe.
Inasemekana polo alimwendea pasta huyo na kumtandika vilivyo akimlaumu kwa kusambaratisha mipango yake.
Pasta aliokolewa na wapita njia naye polo akaonywa dhidi ya kuvuruga amani katika jamii.