• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
COVID-19: Vyama vya kuinuana ‘Chamaa’ pia vyaathirika

COVID-19: Vyama vya kuinuana ‘Chamaa’ pia vyaathirika

Na GEOFFREY ANENE

“KWA mwanachama mpendwa, unafahamishwa kwamba kutokana na janga la coronavirus, mikutano ya chama chetu cha Senje Self Help Group imeahirishwa hadi mtakapofahamishwa tena.”

Huo ni ujumbe mmoja tu unaodhihirisha kuwa hata vyama ambavyo Wakenya wamekuwa wakitumia kujikimu kimaisha kwa kukutana kila mwezi vimeathirika na virusi hatari vya coronavirus, ambavyo kufikia Alhamisi vilikuwa vimeathiri zaidi ya watu 225,000 kote duniani na kusababisha vifo vya watu 9,000.

Kenya imeshuhudia watu saba wakiambukizwa virusi hivyo vinavyoenea kwa haraka. Na kufuatia tangazo la Rais Uhuru Kenyatta mwishoni mwa juma lililopita kuwa mikusanyiko ya watu imepigwa marufuku ili kupunguza uenezaji wa virusi hivyo, sekta mbalimbali zimekuwa zikitoa matangazo kuarifu watu wao kufuata maagizo hayo.

Vyama vya kuwekeza, ambavyo vimepata umaarufu nchini Kenya kama ‘Chamaa’, sasa vimefuata mkondo huo jinsi ujumbe huo ulivyoelekeza. Wanachama wa Senje Self Help Group kutoka Kaunti ya Kakamega walikuwa wakikutana Jumamosi ya pili kila mwezi na kuchanga Sh1,000 kila mmoja.

“Wanachama wetu sasa wameacha kutoa fedha kwa sababu wanadai kuwa walitoka kazini kabla hawajalipwa na pia mwisho wa mwezi haukuwa umefika. Wale walikuwa na mikopo tayari pia wameanza kukwama kuilipa,” alisema Juddy, ambaye ni mwalimu katika shule moja mtaani Kariobangi South jijini Nairobi.

“Tulikuwa tukikutana kila Jumapili ya pili kila mwezi. Sisi kama binamu tulikuwa tumeanzisha chama hicho ili kitusaidie kuimarisha hali zetu za kifedha na pia kimaendeleo. Kila mtu huchangia Sh5,000 kila tunapokutana. Tumeungana binamu 20 katika chama hicho,” aliongeza.

Lydia, ambaye anafanya kazi na shirika moja kubwa la michezo humu nchini, ni mwekezaji katika vyama viwili.

Alisema, “Katika chama chetu cha Rugurus Investment, tulikuwa tukikutana kila Jumapili baada ya kutoka kanisani. Marufuku ya mikusanyiko imefanya tusimamishe mikutano hiyo na sasa tunatuma pesa kwa kutumia huduma za Mpesa. ”

Akaongeza: “Katika chama hicho kingine, ambacho kinaleta pamoja kinamama kutoka makanisa mbalimbali, tulikuwa tunakutana mara mbili kwa mwezi. Hatuwezi kukutana sasa kwa sababu ya amri ya Rais na pia usalama wetu.”

Aidha, watu wengi wanasema virusi vya corona vimewaletea masaibu makubwa kwa sababu hawezi kufika maeneo yao ya kazi.

Naye Maggie, ameeleza ‘Taifa Leo’ kuwa ameathirika kimawazo.

“Nawaza jinsi watoto wangu wataathrika kimasomo. Pia, hali hii imenifanya nitengane nao kwa sababu imenibidi niwapeleke mashambani kwa mamangu angaa huko watakuwa salama kidogo. Vilevile, najutia kulipa karo ya shule ambayo haitawasaidia hata kidogo kwa sababu huwa hairudishwi. Yaani siamini fedha hizo zimeenda tu na maji,” anasema.

You can share this post!

Meneja wa Diamond Platnumz agundulika kuugua Covid-19

COVID-19: Visa vya maambukizi nchini vyasalia saba

adminleo