MAWAIDHA YA KIISLAMU: Kumcha Mungu kuna faida nyingi ikiwemo kuepusha mja na balaa

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Allah.

Mola wetu anapotuamrisha jambo jema basi lina maslaha kwetu sisi. Na anapotukataza jambo baya pia lina maslaha kwetu sisi.

Basi ikiwa ndivyo hivyo inamaanisha kuwa Mola wetu angelijua kama kuna jambo jingine kubwa zaidi na lenye kuleta faida au manufaa kwetu kuliko hili la “Kumcha Mungu” basi bila shaka asingetuficha bali angelituusia ili tupate kutekeleza na lituongoze katika njia Yake na kuokoka na adhabu zake.

Kwa vile Mola wetu ni mjuzi wa kila kitu, kinachofichikana na kinachoonekana ulimwenguni, na kwa kuwa Mola anawatakia kheri waja Wake hivyo kajua ya kwamba hakuna jambo bora zaidi kwa wanadamu kuliko kumcha Mungu.

Nalo ni juu ya yote na sio mwisho wa yote. Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu S.W.T. kawaamrisha waja wake wote kumcha Mungu katika Qurani Tukufu basi si vingine isipokuwa kusudio lake ni kuwapima kwa kuwafanyia mitihani na majaribio ya kutii na kuasi, ili uwepo ushahidi kamili juu yao, na kwa wale waja wanao mcha-Mungu, Mola wao huwafungulia milango ya kheri zote za duniani na za Akhera.

Na kheri hizo za duniani na za akhera zinamkaribisha na kuwa karibu zaidi na Mola wake na kupata radhi zake, upendo wake kisha kupandishwa daraja yake juu zaidi kuliko hata ya viumbe watukufu Malaika. Ndio maana Mwenyezi Mungu S.W.T. amemwamrisha kila Mwislamu amche Mola wake kwa kadiri ya juhudi za ukomo na mwisho wa uwezo wake wote.

Na binadamu ajue kwamba hakika ya uchaji Mungu si kitu kingine bali ni kuiepusha nafsi yake kufanya madhambi yatakayomwangamiza yeye mwenyewe.

Mwishowe humfanya mja yule akawa na azma ya nguvu ya kujizuia baina yake na baina ya dhambi, na hii ndio maana hasa ya kumcha Mungu yaani ni “kizuizi au kinga.”

Kwa mtu yule atakaemuasi na kutokufuata sheria za Mola wake, basi akae akijua kwamba adhabu za Mola Mtukufu ni kali na hatakuwa na uwezo wa kuepukana nazo. Kwa hivyo ni bora kwake mja ajiepushe na adhabu hizo kwa kumtii na kumcha Mola wake. Na kama tutakavyoona katika maelezo ya hapo chini faida za kumcha Mungu ni nyingi sana. Na ushahidi huu ni kutokana na aya nyingi ndani ya Qurani Tukufu. Nazo ni kama zifuatazo. Lakini kwanza kabisa tutaanza kutoa aya ambayo inatuhadharisha sisi sote, nayo ni ya adhabu kwa yule ambaye atamuasi Mola wake. Kwa sababu siku ya kiyama atasimamishwa mbele yake na kumlipa kwa ukamilifu yote yale aliyoyatenda. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Surat Aali-`Imraan aya ya 102, “

Maana yake, “Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa kwa ukamilifu yote iliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa.”

Faida za kumcha Mwenyezi Mungu S.W.T. ni nyingi kupita kiasi lakini kwa kurahisisha mambo hapa nitazitaja kwa uchache tu.

1) Mwenyezi Mungu amemuahidi anayemcha kuwa hawezi kumtupa bali atamheshimu na kumjali kuliko watu wote wale wasiomcha Mungu. Kwa dalili ya Qurani, kasema katika Suratil Hujuraat aya ya 13, “

Maana yake, “…Hakika aheshimiwae sana miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi…”

2) Mola Subhaanahu Wataala humuokoa Mwislamu mcha Mungu katika kila balaa itakayompata hapa duniani na kumwepusha nayo mbali na balaa hiyo, wakati ambapo yeye mwenyewe atashangaa na pengine kwa ule mshangao wake asiweze kuamini vipi ameweza kuokoka nayo. Kwa hali hiyo ucha Mungu ni kinga za balaa na uokovu kwake. Kama alivyotuhadithia Mwenyezi Mungu Subhaanahu Wataala katika Surat Talaaq aya ya 2, “

Maana yake, “…Na anayemcha (anayemuogopa) Mwenyezi Mungu, (Allah) humtengenezea njia ya kuokoka (katika kila balaa).”

3) Mwenyezi Mungu Subhaanahu Wataala. humrahisishia mchaMungu mambo yake yote hapa duniani yamwendee na kuyaona mepesi kwake bila kuhangaika na kupata taabu yoyote ile. Kama alivyotufahamisha katika Surat Talaaq aya ya 4, “

“…Na anayemuogopa Mwenyezi Mungu, (Mola) humfanyia mambo yake kuwa mepesi.”

4) Mwenyezi Mungu Subhaanahu Wataala, amewasifu na kuwapongeza wacha Mungu kwa subira zao na khofu ya kumuogopa Mola wao, na mfano wa Kiswahili unasema “Mstahamilivu hula mbivu.” Kama alivyotuelezea katika Surat Aali-`Imraani aya ya 186, “

Maana yake, “…Na ikiwa mtasubiri na mkamcha (Mwenyezi Mungu), basi haya ni katika mambo muhimu sana ya kufanywa (na watu).”

5) Mola Subhaanahu Wataala amewadhamini wote wale wacha Mungu ikiwa wao watasubiri na kumcha Yeye tu, basi hila za adui au mchawi au hasidi yeyote yule hazitawadhuru. Kwani Mwenyezi Mungu anaona yote wanayoyatenda Binaadamu na Majini na Yeye Ndie Mwenye kuwahifadhi na kila aina ya balaa. Kama alivyotusimulia katika Surat Aali- `Imraani aya ya 120, “Maana yake, “…Na ikiwa mtasubiri na mkamcha (Mwenyezi Mungu basi), hila zao (maadui) hazitakudhuruni.”

6) Mwenyezi Mungu Subhaanahu Wataala, anawatia moyo wale wachaMungu pamoja na wafanyao wema kwamba Yeye daima yupo nao, wasikate tamaa bali wazidi kumtegemea Yeye na atawanusuru na kuwasaidia kwa kila jambo au tatizo litakalowapata. Kama alivyowaahidi katika Suratin Nahl aya ya 128, “

Maana yake, “Kwa hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wale wanaomcha, na wale wafanyao wema.”

7) Mola Subhaanahu Wataala. humsamehe mcha Mungu madhambi yake na kumzidishia ujira wake siku ya Kiyama. Kama alivyomwambia katika Surat Talaaq aya ya 5, “

Maana yake, “…Na anayemcha Mwenyezi Mungu humfutia maovu (madhambi) yake na humpa ujira mkubwa.”

8) Allah Subhaanahu Wataala anawapa moyo wacha Mungu kwamba Yeye anawapenda sana kuliko wengine kwa sababu ya vile vitendo vyao vizuri wanavyovifanya, na kwa kule kumheshimu Mola wao inavyotakiwa. Kama alivyotuelezea katika Surat Tawba aya ya 7, “

Maana yake, “…Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanaomcha (wanaomuogopa).”

9) Mwenyezi Mungu S.W.T. huwatumia wacha Mungu Malaika Wake kwa kuwapa khabari njema wakati ule wa kufikwa na mauti kwamba wasiwe na khofu wala huzuni kwa kuiaga dunia na kuwaacha kama vile: Wake zao na mali yao na watoto wao na jirani zao; kwani Mola wao atawabadilishia kwa mambo mazuri zaidi kuliko hayo ikiwa pamoja na kuwaingiza katika Pepo Yake. Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Yuunus aya ya 63 na ya 64, “

Maana yake, “Wale ambao wameamini na wakawa wanamcha Mungu (wanafuata amri Zake na wanajiepusha na makatazo Yake). Wao wana mema katika maisha ya duniani na katika Akhera…”

10) Mwenyezi Mungu S.W.T. amewadhamini wacha Mungu kwamba wasiwe na khofu yoyote ile atawaokoa na Moto wa Jahannam na watakuwa mbali nao. Kama alivyowaahidi katika Surat Maryam aya ya 72, “Maana yake, “Kisha tutawaokoa (katika Moto) wale wamchao (Mungu); na tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti.”

11) Mwenyezi Mungu S.W.T. hakuusia umma huu peke yake kumcha Mungu bali hata umma zilizopita za kale za watu wa Kitabu yaani Mayahudi na Manasara ziliusiwa kama vile sisi. Kwa hali hiyo yeyote yule atakaetekeleza usia huo na kafuata amri ya Mola wake matokeo yake ataepukana na adhabu zake. Kama alivyotuusia Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratin Nisaa aya ya 131, “

Maana yake, “…Na kwa yakini tuliwausia waliopewa Kitabu kabla yenu, na nyinyi (pia), kwamba mumche Mwenyezi Mungu…

Habari zinazohusiana na hii