KIKOLEZO: Corona yapiga stopu showbiz
Na THOMAS MATIKO
MKURUPUKO wa homa hatari ya virusi vya corona uliozukia China Desemba 2019 na kisha kusambaa kote duniani, umeendelea kuvuruga kila sekta ikiwemo tasnia ya burudani.
Hapa nchini shoo kadhaa tayari zimeaathirika na hata kuwaacha waandalizi wakikadiria hasara. Hizi hapa ni baadhi tu ya shoo za kibabe zilizopigwa stopu na corona. Ni shoo zilizokuwa zimeratibiwa kufanyika lakini kutokana na homa hiyo, zikalazimika kuahirishwa.
CHURCHILL SHOW
Huwa ni shoo ya laivu ambayo hurekodiwa kila wiki. Hata hivyo kwa mara ya kwanza wiki iliyopita, shoo iliyokuwa imeratibiwa kufanyika katika viwanja vya MOW Sports Club, South C, Nairobi haikufanyika kama ilivyo desturi baada ya serikali kutangaza kupiga marufuku mikusanyiko yoyote ya hadhara.
Hivyo ilimlazimu Churchill kurekodi shoo hiyo bila mashabiki ukumbini kwa ajili ya kuzalishia kipindi runinga ya NTV ambayo hupeperusha shoo hiyo.
Uamuzi huo unasemekana kumwingizia hasara kubwa na huenda mtindo ukawa huo huo kwa kipindi cha wiki chache zijazo.
JOHNNIE WALKER MAGICAL KENYA OPEN
Shindano kubwa zaidi la gofu nchini Kenya, Magical Kenya lilitarajiwa kuanzisha rasmi msururu wa parte after parte wikendi iliyopita. Kwa kawaida shindano hilo la siku tatu huwa na shoo za burudani kila jioni kwa siku zote hizo na makala haya hayangekuwa tofauti.
Mmoja wa wadhamini Johnnie Walker alikuwa na ratiba ya shoo nne toka Machi 12. Mashindano hayo yangeanza na kufululiza wikendi nzima.
Alhamisi Machi 12 siku ya kwanza ya shindano, kuliratibiwa kufanyika kwa shoo ya Johnnie Walker Jazz Night katika uwanja wa Karen Country club.
Siku ya pili shoo iliyoratibiwa ilikuwa ya Johnnie Walker Motown Concert, kisha Jumamosi ifuate shoo yua Johnnie Walker Lost in the 90s, manahodha wakiwa Sauti Sol.
Siku ya nne na ya mwisho, Johnnie Walker After Party, Nyashinski na rapa Fena Gitu walitakiwa kupanda jukwani. Shoo zote hizi za kibabe, corona ikapiga stopu.
NAI-FEST (NAIROBI FESTIVAL)
Baada ya kufanikiwa kwa makala ya kwanza ya Nai-Fest mwaka jana yaliyomleta staa wa Nigeria JoeBoy nchini, mwaka huu mwandalizi wa tamasha hiyo soshiolaiti Bridget Achieng alipanga kumleta nyota mwingine kutoka Nigeria Reekado Banks.
Makala hayo ya pili ya Nai-Fest mwaka huu yalikuwa yameratibiwa kufanyika Aprili 4, 2020, lakini sasa yameahirishwa huku waandalizi wakikosa kutangaza tarehe mpya.
Tayari nyota huyo wa Nigeria na wasanii wengine waliopangwa kwenye kikosi cha watumbuizaji walikuwa wameshalipwa kianzio.
GENGETONE FESTIVAL
Kwa mara ya kwanza toka kuchipuke kwa mtindo mpya wa muziki wa Gengetone mapema mwaka jana, 2020 iliratibiwa kufanyika makala ya kwanza ya sherehe za muziki huu ambapo ni wasanii wote wa mtindo huu wangepata fursa ya kufanya makamuzi.
Shoo hiyo ilikuwa imeratibiwa kufanyika mjini Machakos Aprili 10, 2020, lakini mwandalizi ameeleza safu hii kwamba kutokana na corona, wamelazimika kusogeza mbele hadi Mei 2, 2020.
KHANGA FESTIVAL
Ni tamasha ya uswahilini ambayo iliratibiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Aprili 12 katika kaunti ya Kilifi.
Tamasha hiyo ingewapandisha kwenye jukwaa moja wanamuziki, wavunja mbavu, malenga, wanasarakasi, wachoraji na wasanii wengine wa aina aina ikiwa ni sehemu ya kusherehekea utamaduni wa Kenya, pamoja na sanaa.
Tamasha hiyo sasa imeahirishwa na itafanyika mwishoni mwa mwaka 2020.
THE NAIROBI ORCHESTRA CONCERT
Shoo hiii iliratibiwa kufanyika kwa siku mbili wikendi iliyopita Jumamosi na Jumapili katika ukumbi wa Braeside Auditorium kule Lavington.
Hata hivyo kutokana na homa hii, waandalizi waliamua kuifutilia mbali.