KFS yaimarisha doria kuilinda misitu
Na MAGDALENE WANJA
MAAFISA wa Shirika la Huduma ya Misitu Nchini (KFS) wameshika doria kuilinda misitu ikiwa ni njia ya kukabiliana na ongezeko la biashara ya magendo inayohusisha bidhaa zitokanazo na misitu.
Kulingana na msimamizi mkuu wa idara ya uhifadhi Bw Julius Kamau, kisa cha hivi punde kilifanyika Machi 14, 2020, ambapo washukiwa wanne walikamatwa wakijaribu kusafirisha makaa kutoka nchini Tanzania.
Kulingana na Bw Kamau, magunia 400 ya makaa yalinaswa katika tukio hilo ambapo makaa yalikuwa yakiingizwa nchini kupitia njia za kimagendo kwa kutumia pikipiki.
“Afisa wa KFS aliyekuwa katika zamu katika kituo cha Hororo Border Patrol, alipata habari kuhusu lori hilo lililokuwa likipakiwa makaa ndani ya msitu mita 500 kutoka kwa mpaka wa Kenya-Tanzania na ndipo tukachukua hatua ya kuelekea katika eneo hilo,” alisema Bw Kamau.
Bw Kamau alisema kuwa hiki ni kimojawapo cha visa ambapo watu wanaohusika katika biashara hizo wamekuwa wakikwepa kulipa kodi na kujihusisha na biashara hiyo.
Alisema kuwa wash kiwa Hao walifikishwa mahakamani Jumatatu ambapo walitozwa faini ya Sh15,000 kila mmoja.
Lori lenye nambari za usajili linaloaminika kuwa ni la Kaunti ya Kwale ndilo lilikuwa likitumika kufanya biashara hiyo ya magendo.