• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
DAU LA MAISHA: Aliacha kazi ya benki kupigana na ukeketaji

DAU LA MAISHA: Aliacha kazi ya benki kupigana na ukeketaji

Na PAULINE ONGAJI

LICHA ya kuwa hajakumbana ana kwa ana na madhara yanayotokana na ukeketaji, Wanjiru Wahome amejitwika jukumu la kupambana na utamaduni huu.

Ni mwito uliomsukuma kuacha kazi yake katika benki moja jijini Nairobi na kufunganya virago kuelekea Kaunti ya Samburu ili kuhudumia wasichana ambao wanazidi kuteseka kutokana na utamaduni huu.

Huu ukiwa mwaka wake wa saba akihudumu kama afisa wa mipango katika hazina ya Samburu Girls Foundation, kazi yake hasa inahusisha kutafuta ufadhili kutoka kwa wahisani, vile vile kuandika mapendekezo ya kuwezesha shirika hili kupata usaidizi.

Lakini ni shughuli za moja kwa moja za hazina hii ambazo zimekuwa zikimpa Bi Wahome kichocheo cha kuendelea na mwito huu.

Amekuwa akijihusisha vilivyo katika shughuli za kuwaokoa wasichana sio tu kutokana na ukeketaji, bali pia ndoa za mapema.

Ni harakati ambazo zimempeleka katika sehemu mbalimbali eneo hili, huku azma ikiwa kuwafunza wakazi kuhusu athari zinazotokana na ukeketaji.

Lakini pia wamekuwa wakitoa hifadhi kwa wasichana wanaotoroka nyumbani kuepuka ukeketaji na kuozwa mapema.

“Utamaduni huu umekithiri sana katika eneo hili na ndiposa makao ya aina hii yanawasaidia sana wasichana ambao msimamo wao kuhusiana na ukeketaji unakinzana na kauli za jamaa zao,” asema.

Pia, huduma yao imekuwa ikihusisha kutoa ushauri nasaha kwa baadhi ya wasichana hawa.

“Kwa mfano, kulikuwa na kisa cha msichana wa miaka tisa aliyekuwa amekeketwa na alikuwa anapangiwa kuozwa kwa mwanamume wa miaka 38. Alikuja hapa kidonda chake kikiwa bado bichi ambapo alikuwa na uchungu mwingi sana. Kwa msichana wa aina hii, bali na kupokea matibabu ya kimwili, lazima apate ushauri nasaha kwani pia ana majeraha ya kisaikolojia,” aeleza.

Aidha, wamekuwa wakishirikiana na shule tofauti kusaidia wanafunzi kutoka familia maskini kwa kuwapa ruzuku ya karo. “Ni suala ambalo pia tumeweza kufanikisha kutokana na usaidizi wa wahisani,” asema.

Mbali na hayo, wamekuwa wakitoa mafunzo ya mambo ya kawaida maishani kama vile jinsi ya kudumisha usafi, vile vile mawasiliano kwa lugha ya Kiswahili.

Kulingana na Bi Wahome, ari yake ya kutaka kujihusisha katika vita hivi lilimjia baada ya kukutana na bibi mmoja aliyekuwa akisimulia jinsi alivyoozwa akiwa na miaka 11 baada ya kukeketwa.

“Aidha, niliona kwamba kukaa kwangu jijini Nairobi hakukuwa na mchango mkubwa katika jamii, na hivyo niliposikia kuhusu kisa hiki, nilitaka kujihusisha na shughuli ambayo ingeleta mabadiliko katika jamii,” aeleza.

Anajivunia kuchangia kuokoa zaidi ya wasichana 1,500 huku kwa sasa shirika hili likiendelea kawashughulikia wengine 440.

Ni mradi ambao umezaa matunda mema katika jamii hii kwani bali na kubadili mtazamo wa jamii kuhusiana na ukeketaji, umeongeza idadi ya wasichana ambao wamekamilisha masomo.

“Hii imepunguza visa vya ukeketaji katika eneo hili. Aidha, wasichana wengi ambao wamenufaika wamekuwa wakirejea pia kutoa mchango wao kama mfano mwema katika jamii.”

Lakini anakiri ni safari ambayo imekuwa na changamoto kibao.

“Sio rahisi kufikisha ujumbe na kushawishi jamii kuhusu madhara ya ukeketaji. Sio rahisi kushawishi watu kuacha jambo ambalo wamezoea kulifanya tokea kale,” aeleza.

Pia kumekuwa na changamoto ya kufuatilia kesi dhidi ya watekelezaji unyama huu kortini.

“Kesi nyingi zimekuwa zikichukua muda mrefu kuamuliwa mahakamani, suala ambalo linavunja moyo,” asema.

Lakini licha ya haya Bi Wahome hajaonesha ishara za kulegeza kamba katika vita hivi huku akiongeza kwamba furaha yake ni kuona wasichana hawa wanapata usaidizi na kujistawisha kimaisha.

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Mtetezi mahiri wa haki za wanawake

UMBEA: Si vizuri kuficha hasira, yaweza kugeuka shubiri...

adminleo