MWANASIASA NGANGARI: Waziri, mbunge machachari aliyekuwa mtetezi wa Moi
Na KEYB
‘MWENYEKITI’, jina ambalo Elijah Wasike Mwangale alifahamika na wengi, lilibuniwa na Rais Daniel arap Moi alipokuwa Makamu wa Rais na kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.
Mwangale alimpatia Moi wakati mgumu katika vikao vya Bunge kama mkosoaji wa serikali wakati wa utawala wa Rais Jomo Kenyatta.
Baadaye alibadilika kuwa mtetezi mkubwa wa Moi, makamu wa rais alipotwaa mamlaka baada ya kifo cha Kenyatta 1978.
Matukio yaliyopelekea Mwangale kuitwa ‘Mwenyekiti’ yalikuwa mkasa na yahusu mauaji ya kikatili ya aliyekuwa mbunge wa Nyandarua Kaskazini Josiah Mwangi Kariuki (maarufu kama JM), ambaye mwili wake ulipatikana na mfugaji wa jamii ya Wamaasai Ngong Hills karibu na Nairobi mnamo Machi 2, 1975.
Mwangale, wakati huo akiwa mbunge machachari wa Bungoma Mashariki aliyekuwa akifunga ndefu, alisimamia kamati ya watu 11 iliyochunguza mauaji ya JM.
Mwangale aliitwa Ikulu kuhusu ripoti ya kamati hiyo, iliyopendekeza polisi wawachunguze maafisa wawili wa serikali.
Wakati Mwangale na kamati yake waliitwa Ikulu, mwanachama mmoja alibaki nyuma akiwa na nakala halisi ya ripoti hiyo.
Na alipoiwasilisha Bungeni, mbunge huyo alitoa nakala yake na kusema ilikuwa tofauti na iliyowasilishwa.
Spika wa Bunge la Taifa wakati huo, Fred Mati, aliamua kuwa suala hilo lingeibuliwa wakati wa mjadala kama ushahidi- jambo ambalo halikufanyika kwa sababu kulikuwa na hofu ya kuzuiliwa gerezani bila mashtaka wakati huo.
Wakati wa kupigia kura ripoti hiyo, Moi, Mwanasheria Mkuu, Charles Njonjo, na wanasiasa kadhaa walishawishi Bunge kukataa ripoti hiyo- kumaanisha hakuna hatua zaidi ambazo zingechukuliwa. Hata hivyo iliidhinishwa huku Masinde Muliro, waziri wa serikali, na Peter Kibisu, waziri msaidizi, wakikaidi serikali.
Wawili hao walipigwa kalamu siku hiyo, kabla ya Mwangale kujawa na hisia, kuwasilisha mswada wa kukubali ripoti hiyo na kumalizia kwa methali ya Waluhya- mtaalamu huyo wa kilimo aliyesomea Amerika kabla ya kuwa mwanasiasa alipenda kutumia methali.
Jukumu la Mwangale la kusimamia kamati hiyo na kuifanya iidhinishwe na Bunge ilipelekea jina ‘Mwenyekiti’ kudumu. Punde tu baada ya uchaguzi mkuu wa 1979, uliokuwa wa kwanza chini ya utawala wa Moi, Mwangale aliteuliwa waziri wa Leba. Baadaye alihamishiwa wizara za Utalii na Wanyamapori, mashauri ya kigeni na Kilimo.
Ilichukuliwa kuwa aliteuliwa kuongoza wizara hizi kama njia moja ya Moi kumzima. Mwangale alikuwa waziri mwenye ushawishi mkubwa katika jamii ya Waluhya baada ya Moses Mudavadi.
Ingawa alikuwa mwana wa mzee wa kanisa la Friends Church kutoka kijiji cha Matili eneo la Kamukuywa, wilaya ya Bungoma (wakati huu ni kaunti ya Bungoma), Mwangale alikuwa mmoja wa wanasiasa waliofahamika kama vibaraka wa Kanu; wandani wa Moi ambao walikuwa na nguvu nyingi na watetezi sugu wa utawala wa chama kimoja cha Kanu.
Alipoteuliwa waziri wa Leba, Mwangale alianza kushughulikia mgogoro kati ya Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Juma Boy, na wapinzani walioongozwa na Yunis Ismail, aliyekuwa amemuondoa katika chama cha Dock Workers’ Union katika juhudi za kumzuia kutetea wadhifa wake kama Katibu Mkuu katika ngazi ya taifa.
Mwangale aliita Bodi Kuu la COTU na akatisha kuvunja muungano huo iwapo mgogoro ungeendelea hatua ambayo ilituliza hali.
Ilikuwa ni wakati wake katika wizara hiyo ambapo chama cha kutetea wafanyakazi wa umma ambacho katibu wake mkuu alikuwa ni Kimani wa Nyoike, kilipigwa marufuku.
Mwangale alishawishi Moi kwamba watumishi wa umma walikuwa wakitoa huduma muhimu kwa taifa na kwa hivyo, hawakufaa kuwa na uhuru wa kuitisha mgomo kwa sababu hatua hiyo ingelemaza huduma na kuumiza Wakenya.
Waziri huyo alibadilika kuwa mtetezi mashuhuri wa Moi hivi kwamba alifaulu kuangusha miamba wa kisiasa kutoka mkoa wa Kati ambao walichukuliwa kuwa tisho kwa serikali.
Wakati Njonjo, Mwanasheria Mkuu wakati wa mpito alipomsaidia Moi kuingia Ikulu baada ya kifo cha Kenyatta, alipata nguvu. Yeye na G.G. Kariuki, waziri mwingine mwenye nguvu walikuwa watu wa pekee kubebwa katika gari rasmi la kiongozi wa taifa.
Kisha mwaka wa 1983, Moi alizuru wilaya ya Kisii na kuanzisha mjadala wa kuwepo kwa “msaliti” serikalini. Alidai kwamba kulikuwa na mtu aliyesaidiwa na nchi za kigeni kupindua serikali yake.
Mjadala huo uliendelea kwa muda bila jina lolote kutajwa hadi Njonjo aliporejea nchini kutoka ziara ya ng’ambo.
Ni Mwangale akiwa bungeni aliyemtaja Mwanasheria Mkuu kama msaliti aliyekuwa akizungumziwa na kusababisha Moi kuteua Jaji Cecil Miller kusimamia Tume ya Mahakama ya kuchunguza madai hayo.
Tume hiyo ilimwondolea Njonjo lawama dhidi yake lakini wakati huo umaarufu wake kisiasa ulikuwa umefifia.
Baada ya uchaguzi wa ghafla wa 1983, Mwangale alituzwa kwa kuhamishwa kutoka wizara ya Utalii na Wanyamapori hadi wizara ya Mashauri ya Kigeni.
Kabla ya kura ya Mlolongo mwaka wa 1988, kulikuwa na kampeni ya kumtaka Moi kumuondoa Mwai Kibaki kama Makamu Rais.
Vibaraka wa Kanu walimlaumu Kibaki kwa kutoonyesha uaminifu wa dhati kwa chama hicho tawala. Kwa mfano walisema kuwa hakuwa akivaa beji iliyokuwa na picha ya Moi kwenye koti lake ilivyokuwa mtindo. Badala yake, alivaa iliyokuwa na alama ya Kanu.
Mwangale alizuru wilaya ya Nyeri alikotoka Kibaki katika kile kilichoonekana kama kampeni ya kumpinga makamu wa Rais na kumfanya Kibaki kutangaza kuwa hakukuwa na nafasi ya watalii wa kisiasa katika wilaya ya Nyeri. Vilevile, Kibaki alijibu juhudi za kumbandua kutoka kitini chake cha ubunge cha Othaya akisema “kuiba kura kunahitaji kiwango fulani cha werevu.”
Alipoteua baraza lake la mawaziri baada ya uchaguzi mkuu wa 1989, Moi alimfuta Kibaki kama makamu rais na kumteua waziri wa afya.
Josephat Karanja, aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi na waziri msaidizi aliteuliwa kuchukua nafasi ya Mwai Kibaki. Karanja hakuhudumu sana na alifutwa kwa kujigamba alikuwa kaimu Rais Moi alipokuwa ng’ambo. Moi aliporudi, alikariri kwamba alikuwa rais hata akiwa usingizini au nje ya nchi.
Mbunge wa Embakasi David Mwenje, aliwasilisha mswada wa kumuondoa Karanja ofisini na huo ukawa mwisho wa maisha yake ya kisiasa.
Mwangale aliteuliwa waziri wa mashauri ya kigeni wakati wa mizozo ya kieneo na kimataifa. Kulikuwa na mgogoro wa kisiasa Uganda huku mapinduzi yakifuatwa na mapinduzi na kutumbukiza nchi katika taharuki.
Kibarua kigumu kwake kilikuwa Uganda ambayo haikuwa na amani tangu 1975 wakati Idi Amin, afisa wa jeshi, alipopindua serikali ya Milton Obote. Serikali ya pili ya Obote iliyumba 1985, wanajeshi wa serikali walipochoka kupigana na waasi wa National Resistance Movement walioongozwa na Yoweri Museveni.
Jenerali Tito Okello alifanya mapinduzi kisha akajitokeza hadharani kusema “hayakuwa mapinduzi, lakini ni wanajeshi waliokuwa wakizunguka bila mpangilio” jijini Kampala. Hii ilikuwa kumsaidia Obote kuondoka salama kupitia Busia na kuingia Ikulu ndogo ya Kakamega.
Okello, mara moja alitangaza Uganda ilikuwa na serikali mpya akiwa rais. Ilikuwa ni Mwangale aliyetumwa na Moi hadi Kakamega kumsindikiza Obote hadi ikulu ya Nakuru.
Baadaye, Mwangale alikiri hadharani kwamba hakujua iwapo alipaswa kumtambua Obote kama “Mtukufu aliyekuwa rais au kumwita tu “Dkt Obote.”
Mwangale alihamishiwa wizara ya Kilimo baada ya uchaguzi mkuu uliovurugwa wa 1988 na kumwachia Robert Ouko kusimamia wizara ya mashauri ya kigeni.
Katika wizara ya Kilimo, mhadhiri huyo wa zamani alithibitisha utaalamu wake kwa kuimarisha ufugaji kote nchini. Wakulima wa miwa na mahindi walikuwa wakipata malipo kwa wakati na walikuwa wakipata mbolea bila kuchelewa ili kuimarisha kilimo.
Hadithi ya Mwangale kupanda hadi kilele cha mamlaka inafurahisha sawa na maisha yake ya awali.
Akiwa mvulana mdogo, baba yake alimpeleka shule ya msingi ya Chesamisi lakini hakufurahishwa nayo alipofika kiwango kilichofahamika kama intermediate. Aliamua kuhamia shule nyingine upande wa Uganda lakini akarejea nyumbani baada ya muda mfupi.
Baba yake alimpeleka shule moja Mombasa ambako inasemekana alianza kupenda kilimo. Alisoma masuala ya Kilimo katika Egerton College, karibu na mji wa Nakuru na kuhitimu na Diploma.
Mmoja wa walimu wake alikuwa ni William Odongo Omamo, waziri mwingine aliyehudumu katika serikali ya Kenyatta na Moi.
Omamo alimteua miongoni mwa wanafunzi watatu waliopata ufadhili kwenda kusomea Chuo Kikuu cha Virginia, Amerika kwa sharti kuwa wangerudi kufunza Egerton.
Akiwa America ambapo Mwangale alipata digrii ya kwanza na uzamili, alikutana na mkewe Janet, raia wa Amerika.
Alirudi kufunza Egerton kabla ya kujiunga na siasa na baadaye akaoa mkewe wa pili, Salome.
Akiwa mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa, Mwangale alikosa kutambua wimbi la mabadiliko yaliyojiri na mfumo wa vyama vingi vya kisiasa 1992 ambao ulisomba mibabe wa kisiasa wakakosa kurudi Bungeni.
Kabla ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi, alikuwa amempuuza na kumdharau mpinzani wake, Mukhisa Kituyi, ambaye hakuwa akifahamika sana. Kituyi alikuwa waziri katika serikali ya Rais Kibaki na kwa wakati huu ni Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD).
Kituyi alishinda uchaguzi huo kwa kura nyingi na kumtupa Mwangale aliyekuwa wakati mmoja akielea katika bahari ya mamlaka katika jangwa la kisiasa.
Juhudi za kufufua Mwangale kwa kumteua mwenyekiti wa Shirika la Kukadiria Ubora la Kenya (Kebs) katika mazingira ya kisiasa yaliyobadilika hazikufua dafu.
Mwangale alifariki 2004 akiwa na umri wa miaka 66.
Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke