Wakenya 7,800 wapimwa virusi vya corona

Na COLLINS OMULO

ZAIDI ya watu 7,800 walipimwa jijini Nairobi wikendi kubaini iwapo wana virusi vya corona. Kati ya waliopimwa, 5,328 ni watoto, 2,057 wakiwa watu wazima huku vijana wakiwa 434. Kufikia sasa maradhi ya yanayosababishwa na corona yameua zaidi ya watu 13,000 duniani.

Maeneo yaliyopigwa dawa ya kuua viini ni Kituo cha Posta (GPO), hoteli ya Hilton, kituo cha mabasi cha Kencom, soko la Muthurwa na Aghakan Walk.

Mengine ni kituo cha mabasi cha Khoja, City Market, National Archives, bustani ya Jeevanjee na barabara za Hakati, Tom Mboya, Ronald Ngala na Mfangano.

Waziri wa Afya wa kaunti Hitan Majevdia alisema kwamba wanalenga kunyunyiza dawa hiyo katika kituo cha mabasi cha Railways, Bus station na kituo cha reli hadi mnamo Ijumaa, Machi 27, 2020.

“Tunalenga vituo mbalimbali vya mabasi huku tukilenga kuzima maambukizi ya virusi vya corona ikizingatiwa kwamba watu saba tayari wamepatikana navyo nchini,” akasema Bw Majevdia.

Zaidi ya wahudumu 215 wa afya wa kaunti wamehusishwa kulenga vituo vya mabasi, maeneo ya kupumzika watu jijini, masoko na maeneo ambako watu hukusanyika kupiga gumzo.

Kaunti imetoa ambulensi 13 za kuwasafirisha watu wanaoshukiwa kuwa na virusi hivyo. Saba ya ambulensi hizo zitahudumu katika hospitali za Kibera South, Mathare, Mutuini, Pumwani, Kahawa West na Dandora 2.