CORONA: Treni ya huduma za jijini yapunguza idadi ya abiria
Na GEOFFREY ANENE
WATUMIAJI wa huduma za treni kutoka vituo vya Kariobangi South na Mutindwa watalazimika kutafuta njia mbadala ya usafiri kufika mjini Nairobi asubuhi kufuatia amri ya serikali ya kupunguza idadi ya abiria kwa asilimia 60 kuanzia Machi 23, 2020.
Kwa kawaida, garimoshi hilo linalohudumu kutoka Ruiru katika kaunti ya Kiambu hadi mjini Nairobi kupitia stegi za Githurai, Mwiki, Dandora, Kariobangi South, Mutindwa na Makadara, hubeba kati ya watu 5,500 na 6,000 kila siku katika safari moja kutoka Jumatatu hadi Ijumaa.
Treni hiyo huwa na mabogi 20 ya kubebea abiria, huku kila bogi ikiwa na watu kati ya 100 na 120. Hata hivyo, kufuatia mkurupuko wa ugonjwa Covid-19 unaosababishwa na virusi hatari vya corona, kila bogi sasa inahitajika kuwa na abiria wasiozidi 50.
Hatua hii imeacha mamia ya abiria wa mtaa wa Kariobangi South wakihangaika. Abiria walifika katika kituo cha kuabiri treni hiyo cha KCC kama kawaida mapema Jumatatu, lakini ilipita bila kusimama katika eneo hilo dakika kumi mapema kuliko saa inayopita katika siku inayohudumu ya saa moja na dakika 10 asubuhi.
Wengi wa abiria wanaoingia garimoshi hilo katika mtaa wa Kariobangi South sasa watalazimika kurudi nyuma kung’ang’ania nafasi chache zitakazopatikana katika stegi ya Dandora ama kutumia njia mbadala ya kufika maeneo yao ya kazi, vyuo ama kufanya shughuli zingine zozote mjini.