HabariSiasa

Waiguru ataka Bi Ngirici na mumewe wakamatwe

April 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NICHOLAS KOMU na JOSEPH WANGUI

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru amewataka polisi wamkamate Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo, Wangui Ngirici na mumewe Andrew Ngirici.

Gavana huyo anawashutumu wawili hao kwa madai ya kuwalipa vijana kumpigia kelele wakati Naibu Rais William Ruto alipofanya ziara Kerugoya.

Bi Waiguru alisema wawili hao walisababisha machafuko yaliyomzuia kuhutubia wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari mjini Sagana, gavana huyo alilalamika kuwa baadhi ya wafuasi wake walikamatwa kuhusiana na kisa hicho.

“Nimewataja wawili kuwa wahusika wakuu katika kisa hicho. Polisi wameanza kukamata washukiwa ambao hawakuhusika. Wawili hao waliwalipa vijana kadhaa waliokuwa wamejihami kwa visu ili kuhofisha watu na kutatiza mkutano,” alisema gavana huyo.

“Polisi wanafaa kuambia wakazi ikiwa wawili hao hawawezi kunaswa kwa sababu ya pesa zao.”

Mapema kupitia kwa taarifa katika vyombo vya habari, gavana huyo aliomba msamaha kuhusiana na kisa hicho cha Ijumaa, na kusema lengo lake kuu lilikuwa ni maendeleo na sio siasa.

“Hatua hiyo haikuwa tu ya kibinafsi lakini pia ya kishenzi,” alisema Bw Waiguru.

Msimamizi huyo wa kaunti alipigiwa kelele na baadhi ya vijana wakati wa uzinduzi wa barabara ya kilomita 100 ya Gakoigo kuelekea Njega, Kirinyaga ya kati, katika hafla iliyokuwa ikiendeshwa na Naibu wa Rais William Ruto.

Wakazi wa eneo hilo walimpigia kelele huku tofauti za kisiasa kati ya viongozi eneo hilo zikijitokeza hadharani.

Hotuba ya Bw Ruto ilitatizwa kwa muda mfupi eneo la Kerugoya huku vijana wakiitisha kuondoka kwa gavana huyo kwa kibwagizo: “Waiguru must go.”