• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
TEKNOHAMA: Simu kutumika kukabili Covid-19

TEKNOHAMA: Simu kutumika kukabili Covid-19

Na LEONARD ONYANGO

KATIKA juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, serikali imekuwa ikishauri wananchi kuepuka maeneo yenye msongamano wa watu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kuwa ni sharti kuwa na angalau umbali wa mita moja (futi 3) kati yako na mwenzako.

Hii ni kwa sababu ikiwa umesimama karibu na mtu aliye na virusi vya corona, ni rahisi kuambukizwa endapo atakohoa au kuchemua. Mwathiriwa anapopiga chafya au kukohoa, watu waliokaribu naye hupumua hewa iliyo na chembechembe za virusi vya corona na kuambukizwa.

Ili kuzuia misongamano ya watu, serikali imefunga shule na baadhi ya magavana wamefunga masoko kama njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwake.

Serikali pia imeshauri watu kuepuka kuhudhuria hafla za mazishi, harusi, ibada makanisani/misikitini na mikutano mingineyo isiyokuwa ya lazima.

Lakini baadhi ya watu wamepuuza ushauri huo wa serikali na wangali wanasongamana mazishini, sokoni, kumbi za burudani na maeneo mengineyo.

Serikali ya Amerika sasa inafanya mazungumzo na mitandao wa Facebook na Google katika kutambua maeneo yaliyo na watu wanaoendelea kusongamana kinyume na agizo la serikali.

Rais wa Amerika Donald Trump amepiga marufuku mkutano wa zaidi ya watu 10 huku mwenzake Angela Merkel wa Ujerumani akipiga mkusanyiko wa watu zaidi ya wawili.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa katika mtandao wa habari wa Washington Post, serikali itakuwa ikitumia simu kubaini maeneo yaliyo katika hatari kubwa ya kuambukizwa corona kutokana na msongamano mkubwa wa watu.

Kwa mfano, ikiwa watu zaidi ya 200 wamekusanyika mazishini na wamefungua simu zao, mitandao ya Facebook na Google inakusanya taarifa hizo na kuzituma kwa serikali. Baada ya muda mfupi, maafisa wa polisi wanawasili na kuwatawanya kwa nguvu.

Mitandao ya Facebook na Google pia itatuma taarifa kwa serikali iwapo watu waliojikusanya katika eneo fulani hawajazingatia umbali wa angalau mita moja.

Mitandao ya Google na Facebook hutambua eneo ambapo mtumiaji alipo. Hivyo huwa rahisi kutambua ikiwa watu wengi wako pamoja.

Serikali ya Uingereza inatumia kampuni za kutoa huduma za simu kunasa watu wanaokiuka ushauri wa kuepukana na misongamano ya watu.

Serikali ya Uingereza pia inatumia taarifa hizo kubaini ikiwa watu wamezingatia agizo la kusalia nyumbani ili kuepuka kuambukizwa virusi vya corona au la.

Mataifa ya Israel na Australia pia yanatumia kampuni za simu kubaini misongamano ya watu.

Bunge la Israeli lilipitisha sheria ya kuruhusu serikali kutumia taarifa za simu kuzuia misongamano ya watu. Kadhalika, taarifa hizo za simu zinatumiwa kufuatilia mienendo ya watu waliowahi kutangamana na waathiriwa wa corona.

Kampuni ya huduma za simu, Vodafone tayari inashirikiana na serikali ya Italia kuzuia misongamano ya watu katika eneo la Lombardy ambalo limeathirika pakubwa na maambukizi ya virusi hivyo.

Mbali na misongamano ya watu, shirika la WHO pia linashauri watu kunawa mara kwa mara na kuepuka kugusa macho, pua au mdomo.

Unapogusa macho, mdomo au pua na mikono iliyo na viini, virusi hupenya hadi mwilini na kukufanya kuwa mgonjwa.

Unapohisi dalili za homa ya corona kama vile maumivu ya kichwa, kikohozi kikavu, kutokwa na kamasi na kuhisi joto jingi mwilini, unashauriwa kuepuka kutangamana na watu wengine ili kuzuia maambukizi zaidi.

You can share this post!

Isiolo Starlets walenga ubingwa fainali za Chapa Dimba

PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda kutokana na mafua...

adminleo