• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda kutokana na mafua vinanisumbua

PATA USHAURI WA DKT FLO: Vidonda kutokana na mafua vinanisumbua

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Nitakabiliana vipi na vidonda vinavyotokana na mafua ambavyo vimekuwa vikinikumba puani kila mara?

Sly, Nairobi

Mpendwa Sly,

Vidonda vinavyotokana na mafua husababishwa na virusi vya Herpes Simplex. Watu wengi huambukizwa maradhi haya utotoni kutoka kwa wenzao. Virusi hivi haviponi na badala yake hujificha mwilini na kujitokeza tena ukiwa na mawazo mengi, ukiwa na mafua au iwapo kuna mabadiliko ya kihomoni mwilini. Hauwezi angamiza vidonda hivi kamili, lakini waweza kabiliana navyo kwa kutumia krimu kupunguza maumivu na uvimbe au kutumia dawa za kukabiliana na virusi ili kupunguza muda wa makali ya vidonda hivi. Ikiwa pia una vidonda vya mdomoni, sukuta mchanganyiko wa maji yaliyopashwa moto na chumvi mdomoni, au utumie dawa maalum ya kukabiliana na viini mdomoni (mouth wash), jiepushe na vyakula au vinywaji moto na vyakula vilivyo na chumvi nyingi. Pia kunywa maji mengi na udumishe usafi wa mdomoni. Aidha, huenda ukanufaika kutokana na vijalizo vya vitamini B na asidi ya folic. Ikiwa kidonda kitaendelea kwa zaidi ya majuma mawili bila kupona, basi unahitaji kuchunguzwa na daktari.

Kwa majuma kadhaa sasa nimekuwa na chunusi katika kinena. Nimejaribu kupaka krimu za aina mbalimbali hasa kufuatia ushauri wa wanafamasia, pasipo mafanikio. Nitakabiliana vipi na tatizo hili?

Maurice, Mombasa

Mpendwa Maurice,

Huenda chunusi yenye maumivu ikatokana na kuziba kwa vinyweleo (mahali ambapo nywele huchomoka kwenye ngozi) kutokana na bakteria na vitu vingine, mwasho na au maambukizi ya vinyweleo, nywele zinapokua baada ya kuzinyoa. Mbinu sahili ya kutibu shida hii ni kuacha nywele ziote, au kuzichenga badala ya kuzinyoa kabisa. Unaweza tumia krimu ya kunyoa hizi nywele au kuziondoa kabisa kwa kutumia utaratibu wa kuziondoa kabisa ujulikanao kama laser au electrolysis. Uvimbe unaotokana na nywele zilizoota ndani ya ngozi zaweza ondolewa kwa utaratibu kwa kutumia kibanio (tweezer). Kuna baadhi ya krimu ambazo zaweza saidia kupunguza uvimbe kama vile krimu, dawa za kukabiliana na chunusi, krimu za viua vijasumu endapo kuna maambukizi, vilevile tembe za viua vijasumu ikihitajika.

Chunusi hii yaweza pia kuwa kutokana na maambukizi ya zinaa kama vile kaswende, herpes na kadhalika. Kutokana na sababu kuwa umejaribu kutumia krimu bila mafanikio, litakuwa jambo la busara iwapo utamuona daktari ili ufanyiwe uchunguzi unaofaa na hata kupokea matibabu.

You can share this post!

TEKNOHAMA: Simu kutumika kukabili Covid-19

CORONA: Mapasta na wafuasi wao waumia

adminleo