• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
SEKTA YA ELIMU: Masomo ya redioni, mitandaoni si makamilifu bali ni ya ziada tu

SEKTA YA ELIMU: Masomo ya redioni, mitandaoni si makamilifu bali ni ya ziada tu

Na CHARLES WASONGA

MNAMO Jumatatu wiki hii Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na Shirika la Habari Nchini (KBC) walianza rasmi kutoa mafunzo kupitia kwa redio kwa wanafunzi wa shule za msingi na upili kote nchini.

Vipindi vya mafunzo vinaendeshwa kupitia KBC Redio Taifa, KBC Idhaa ya Kiingereza, sawa na katika idhaa za Iftini FM na Transworld Redio ambazo hupeperusha matangazo katika maeneo ya Garissa, Wajir na Mandera.

Vile vile, vipindi vya masomo vinapeperushwa kupitia runinga ya Edu TV inayomilikiwa na Taasis ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) na kupitia mtandaowa Youtube.

Akitangaza mpango huo wiki jana, baada ya serikali kuamuru shule zote zifungwe ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya korona, Waziri wa Elimu George Magoha alisema mpango huo utahakikisha kuwa “wanafunzi wanaendelea na masomo wakiwa nyumbani.”

Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa KICD Joel Mabonga akasema: “Tuko tayari kuhakikisha kuwa watoto hawaachwi nyuma kimasomo wakati huu ambapo taifa letu linakabiliwa na janga hili.”

Kwa upande wake, Chama cha Wachapishaji Nchini (KPA) kimetangaza kuwa vitabu vya sasa vinaweza kupakuliwa, bila malipo, mitandaoni kupitia tarakilishi au rununulishi (smartphones).

“Hatutatoza ada yoyote kwa vitabu hivyo na tumeiruhusu KICD kuviweka katika mtandao wake ili wanafunzi waweze kuvifikia kupitia kompyuta au simu za mikononi,” akasema Mwenyekiti wa KPA Lawrence Njagi.

Licha ya kuanzishwa kwa mpango huu wa masomo, walimu na wataalamu wanaonya kuwa usichukuliwe kama mafunzo mbadala kwa masomo yale ya kawaida ya darasani.

Walimu tuliozungumza nao kwa ajili ya makala haya walifananisha mafunzo hayo na masomo ya ziada, au ya pembeni, wala si njia ya kitaaluma ya kushughulikia mtaala.

“Shule zitakaporejelea shughuli za masomo, tutaanza kushughulikia mtaala mahala ambapo tuliachia tulipoagizwa kufunga shule kutokana na mchamko wa virusi vya korona licha ya kuwepo kwa mafunzo haya ya redio na televisheni,” anasema John Oluoch ambaye ni mwalimu katika shule moja ya upili jijini Nairobi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (Kepsha) Nicholas Gathemia asema mafunzo yanayoendeshwa kupitia redio, runinga na mitandaoni si makamilifu kama yale yanayoendeshwa madarasani.

“Kitaaluma, mwalimu huandaa mipango ya vipindi vya masomo yaani akitilia maanani uwezo wa mwanafunzi wake kumilisi masomo mbalimbali. Hii ni kwa sababu kimsingi, wanafunzi wote nchini hawana uwezo sawa. Kwa hivyo, hukadiria namna wanafunzi wake wameelewa mada au somo fulani, kwa misingi ya lesson plan,” anasema

Hata hivyo, anapongeza hatua ya kuzinduliwa kwa mpango wa masomo ya ziada akisema “utawasaidia wanafunzi kujifunza dhana chache mpya.”

Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya elimu John Mugo anasema kuwa masomo ya redioni na mitandaoni zaidi ya kuwa na mapungufu mengi kitaaluma hayatawafikia watoto wote nchini.

“Kimsingi, ukweli ni kwamba si familia zote nchini zina redio, runinga, tarakilishi na simu za kisasa zenye uwezo wa kufikia mitandao mbalimbali. Hapa narejelea familia nyingi masikini, haswa zilizoko maeneo kame nchini,” anasema Dkt Mugo akiongeza kuwa baadhi yazo hata hazina redio.

Kauli ya msomi huyu inahimiliwa na matokeo ya sensa ya mwaka jana yanayoonyesha kuwa ni Mkenya mmoja kati ya watano ambao wanatumia intaneti katika shughuli zao za kila siku. Na ni asilimia 10.4 pekee ya Wakenya 47.5 milioni kuanzia umri wa miaka mitatu kuenda juu, hutumia kompyuta.

Na japo jumla ya Wakenya 20.6 milioni wanamiliki simu za mikono, ni asilimia tisa pekee wanaomiliki simu zenye mitandao.

You can share this post!

Mshukiwa wa uhalifu auawa Kayole

NDIVYO SIVYO: Kudhihaki au kudharau mtu ni kumcheka bali si...

adminleo