• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 3:17 PM
Rais wa Botswana atengwa baada ya ziara nchini Namibia

Rais wa Botswana atengwa baada ya ziara nchini Namibia

Na MASHIRIKA

GABORONE, BOTSWANA

RAIS wa Botswana Mokgweetsi Masisi, amejitenga kwa hiari huku idadi ya walioambukizwa virusi vya corona barani Afrika ikipanda kwa kasi.

Afrika Kusini nayo ilitangaza kafyu ya wiki tatu kote nchini humo kujaribu kuzuia maambukizi zaidi.

Rais Masisi alichukua uamuzi huo baada ya kurejea kutoka nchini Namibia, ambako alikuwa amehudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais Hage Geingob mwishoni wa wiki jana.

Kiongozi huyo wa Botswana alikosolewa zaidi kufuatia uamuzi wake wa kwenda Namibia.

Wakili na mtetezi wa haki za binadamu Uyapo Ndadi alisema: “Hakuna asiyeweza kuambukizwa virusi vya corona. Sharti sote tukome kusafiri nje. Inaudhi kwamba rais wetu alikwenda nje kinyume na agizo lililotolewa na serikali yake.”

Namibia imeripoti visa vitatu pekee vya maambukizi, na inachukuliwa kama taifa ambalo halikabiliwi na hatari ya kuathirika na virusi hivyo.

Kufikia sasa Botswana ni miongoni mwa mataifa machache ya Afrika ambayo hayajaripoti kisa chochote cha maambukizi.

Nchini Afrika Kusini, Rais Cyril Ramaphosa mnamo Jumatatu alitangaza amri ya watu kukaa manyumbani mwao kwa majuma matatu.

Hii ni baada ya idadi ya walioambukizwa kupanda kutoka 61 hadi 402 katika kipindi cha siku sita pekee.

“Serikali imeamuru kwamba hakuna atakayeruhusiwa kuondoka nyumbani kwa siku 21 kuanzia Alhamisi ili kuzuia kuenea kwa janga hili,” akasema Rais Ramaphosa.

Hatua iliyochukuliwa na Afrika Kusini ilijiri siku moja baada ya amri kama hiyo kutolewa na serikali ya Rwanda baada idadi ya maambukizi kufika 36.

Zimbabwe nayo imerekodi kifo cha kwanza kutokana na virusi vya corona baada ya mwanahabari Zororo Makamba kufariki.

Marehemu alikuwa mtu wa pili kuambukizwa nchini humo.

Naye Waziri wa Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameamuru kufungwa kwa mipaka ya nchini ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Hatua hiyo inaashiria kuwa usafirishaji wa bidhaa na watu kutoka mataifa jirani ya Kenya, Djibouti, Somali, Sudan, Sudan Kusini na Eritrea imezimwa.

Mataifa yote majirani ya Ethiopia yameripoti visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Mnamo Jumatatu aliyekuwa makamu wa rais wa Nigeria, Atiku Abubakar alitangaza kuwa mwanawe ameambukizwa ugonjwa uliozuka China mwishoni mwa mwaka jana.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamuziki mwingine Afrika afa kwa Covid-19

Aachiliwa baada ya kuishi rumande siku 15

adminleo