CORONA: Hali duni ya seli za polisi Bonde la Ufa yazua hofu
Na BARNABAS BII
HUKU serikali ikijitahidi kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, wanaharakati wa haki za binadamu na maafisa wa usalama eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wana wasiwasi kwa sababu ya hali mbaya ya baadhi ya seli katika vituo vya polisi.
Wanaharakati wameomba serikali kutenga pesa za kukarabati na kupanua seli za polisi ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona na maradhi mengine ya kuambukizwa.
Baadhi ya maafisa wa vyeo vya juu wa polisi katika eneo hilo walikiri kwamba kuna msongamano katika seli huku katika kaunti za Pokot Magharibi na Turkana washukiwa wakizuiliwa katika seli za muda.
“Majengo kama maghala na karakana bila vyoo na mabafu au taa yamebadilishwa kuwa seli za polisi. Huku ni kukiuka haki za washukiwa kabla ya kushtakiwa,” alisema afisa mmoja wa polisi wa cheo cha juu ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza na wanahabari.
Mwanaharakati wa haki za binadamu Nick Omito alisema mbali na kuwa na msongamano wa wafungwa, seli ziko katika hali mbaya, zinavuja wakati wa mvua, na kukosa au kuharibika kwa vyoo kunafanya washukiwa kutoa hongo.
“Nimetembelea nyingi ya seli za polisi eneo hilo na ziko katika hali ya kusikitisha hivi kwamba washukiwa wanaamua kutoa hongo badala ya mateso ya kisaikolojia wanayopata wakifungiwa seli,” alisema Bw Omito.
Alidai kwamba baadhi ya maafisa wa polisi hushirikiana na wahalifu sugu kuitisha washukiwa hongo ili waachiliwe kutoka seli chafu.
Maafisa wa polisi hawakuweza kukanusha au kukubali madai hayo lakini wakasema kila mshukiwa hupatiwa risiti ya mali wanayopeana kituoni kabla ya kufungiwa seli na hurudishiwa wakipelekwa kortini.
Afisa mmoja wa polisi alisema serikali inafaa kuhakikisha kuwa seli za polisi zinafaa kuwa sehemu ya kubadilisha tabia ya washukiwa na sio kuwafanya wahalifu sugu au kuendeleza ufisadi katika jamii.
“Kwa kawaida, washukiwa wanafaa kushtakiwa ndani ya saa 48 lakini baadhi yao hukubali makosa ambayo hawajafanya na kutoa hongo ili wasifungiwe seli kuteswa na wahalifu sugu, polisi na mazingira duni ya seli zenyewe,” alisema Omito.