Habari Mseto

CORONA: Wachuuzi wafurushwa

March 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

IRENE MUGO na NICHOLAS KOMU

WACHUUZI na wamiliki wa biashara ndogondogo wamefurushwa katika mitaa ya Nyeri ili kupunguza msongamano na mtagusano wa binadamu.

Wachuuzi wote na wamiliki biashara ambao hawana majengo ya kudumu walifukuzwa kutoka mitaa hiyo na kuamrishwa kufunga biashara zao hadi wakati usiojulikana.

Haya yamejiri kufuatia majadiliano baina ya sekta mbalimbali na serikali ya Kaunti, Jumanne jioni.

Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa kutokana na wasiwasi kuhusu msongamano wa watu katika Mtaa wa Gakere Street, eneo lenye shughuli nyingi zaidi mjini Nyeri.

Mapema juma hili, mamlaka ilikuwa imeelezea wasiwasi kuhusu shughuli za wachuuzi huku Kamishna wa Eneo la Kati Wilfred Nyagwanga akihimiza serikali ya kaunti kubuni suluhisho mwafaka la kudhibiti sekta hiyo.

Mtaa huo ulichukuliwa kama kituo hatari huku taifa likipambana kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona nchini.

Mnamo Jumanne jioni, idara ya biashara Kaunti ya Nyeri ilifutilia mbali siku zote za soko na kuamrisha kufungwa kwa biashara zote za muda na zisizo za kudumu.

Wafanyabiashara nje ya Nyeri pia wamepigwa marufuku kuleta mazao yao katika kituo hicho cha kibiashara.

Serikali ya kaunti hiyo pia imepiga marufuku bidhaa zote zinazoagiziwa nje ya kaunti hiyo.

“Mnaarifiwa kuwa siku za soko wazi almaarufu siku za soko ambapo wafanyabiashara kutoka maeneo na kaunti mbalimbali huleta bidhaa zao kuziuza katika masoko ya kaunti, zimepigwa marufuku hadi notisi nyingine itakapotolewa. Amri hii itaanza kutekelezwa mara moja,” alisema waziri wa kaunti hiyo anayehusika na biashara Diana Kendi.

Waziri huyo alisema ni wafanyabishara wenye vituo vya kudumu pekee walivyopatiwa na kaunti watakaoruhusiwa.