CORONA: Biashara ya miraa yapigwa marufuku Lamu kuzuia mikusanyiko
Na KALUME KAZUNGU
WARAIBU wa miraa Kaunti ya Lamu wanahangika kwa kukosa bidhaa hiyo siku moja baada ya serikali kupiga marufuku biashara hiyo kote Lamu kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Mnamo Alhamisi, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alitangaza ni mafuruku kwa magari yanayosambaza miraa Lamu kuendelea kufanya hivyo huku akiagiza vibanda vyote vya kuuzia bidhaa hiyo kufungwa mara moja.
Kulingana na Bw Macharia, tabia ya wauzaji na watafunaji miraa ya kukusanyika pahala pamoja huenda ikachangia pakubwa maambukizi ya maradhi ya Covid-19 eneo hilo.
Aidha utafiti uliofanywa na ‘Taifa Leo’ kufikia Alhamisi umebaini kuwa baadhi ya watafunaji miraa wamelazimika kusafiri hadi kaunti jirani ya Tana River, Kilifi na hata Mombasa kutafuta miraa ilmuradi wakate kiu chao cha uraibu huo.
Aidha wengine wamefikia kiasi cha kuugua wakiwa wamejifungia ndani ya vyumba vyao kutokana na kukosa miraa.
Bw Mohamed Omar, ameitaka serikali kutafuta njia mbadala za kufikisha miraa Lamu kwani waraibu wanaumia pakubwa kwa kukosa bidhaa hiyo.
“Hatua hii ya serikali kufunga ghafla biashara ya miraa imefanya tumebaki nyumbani tukiumwa na mashavu,” akasema Bw Omar.
Naye Bi Khadija Salim naye amesema la muhimu ni kuzingatia usafi wa mwili na mazingira ya watumiaji. Bi Salim aidha amepinga vikali hatua ya kupiga marufuku uuzaji na utafunaji wa miraa Lamu, akidai miraa ndiyo huwasaidia waraibu kutulia nyumbani.
“Angalia sasa marufuku ya miraa yametusukuma kusafiri mbali na karibu kuitafuta, ikiwemo nje ya Lamu; hali inayotuhatarisha sisi wenyewe kuambukizwa virusi vya corona, amesema Bi Salim huku akiiomba serikali iibuke na mbinu mbadala ya kusafirisha miraa hadi Lamu.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Miraa na Muguka, Kaunti ya Lamu, Bw Ibrahim Kamanja, ameunga mkono wito wa waraibu wa miraa kwamba marufuku yaondolewe au kuzinduliwe mbinu mbadala na salama ya kusafirisha miraa hadi Lamu.
Kulingana na Bw Kamanja, wafanyabiashara wa miraa huenda wakafungiwa nyumba zao kwa kukosa kulipa kodi, ikizingatiwa kuwa tegemeo lao la kipekee ni biashara ya miraa.
“Ikiwa hawataki malori yasambaze miraa eneo hili kwa sababu ya corona, serikali yenyewe iibuke na usafiri mbadala na salama utakaofikisha miraa Lamu ili nasi nyumba zisifungwe kwa kukosa kodi,” akasema Bw Kamanja.