Habari Mseto

CORONA: 'Ugonjwa huu umebana maisha yetu'

March 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMUEL BAYA

Kwa miaka mingi maisha ya Bw Nelson Gitonga yalikuwa kama yale ya mkazi wa kawaida tu kijijini. Kwanza alizoea kujumuika na familia na kuendelea kuwa pamoja vijijini, akihudhuria hafla za matanga na hata harusi.

Haya kwa kawaida ndiyo yaliyokuwa maisha yake hadi janga la Corona lilipobisha hodi nchini na kila kitu kikabadilika. Kwa sasa Bw Gitonga ambaye ni mkaazi wa Subukia, kaunti ya Nakuru amelazimika kubalisha hali ya maisha yake kutokana na mwongozo wa serikali.

Kulingana na mwongozo wa wizara ya afya katika kuangamiza janga la Corona, hakuna kusalimiana, wala kukaribiana, jambo ambalo miezi michache nyuma hakuwa akitarajia kwamba litakuwa hivyo.

Anafanya hivyo kwa kuitikia mwito wa wizara ya afya kwamba lazima wakenya wawe makini na kudumisha uasafi wa hali ya juu ili kukabili kusambaa kwa virusi vya Corona.

“Hili janga la Corona sio mchezo na limeharibu kabisa utaratibu wa maisha ambayo tulizoea kuishi miaka ya nyuma. Nimelazimika kubadilisha baadhi ya tabia ambazo nilikuwa nazo miaka ya nyuma kwa ajili ya kukabiliana na janga hili. Siwezi kusalimia mtu kwa mkono. Sili matunda kama ilivyokuwa hapo awali kwa sababu ya hofu kuhusu mahali matunda hayo yalikotoka,” akasema Bw Gitonga.

Vile vile Bw Gitonga amebana mpango wa kununua nguo za mitumba kwa dai hajui usalama wa maeneo ambako zinatoka.

“Kwa sasa siwezi kununua nguo ya mtumba kwa sababu sijui mahali ambapo zilitoka na viwango vya afya. Vile vile hata mfumo wangu wa kula chakula umebadilika,” akasema Bw Gitonga.

“Niko na chakula change nyumbani ambacho ninatumia katiak juhudi za kukwepa maambukizi ya ugonjwa huu,” akasema.

Mkaazi mwengine wa Nakuru Bw Nelson Ongeri, pia amebadilisha mfumo wa maisha katika kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo.

“Mambo mengi yamebadilika sana kutokana na janga hili. Kawaida nilizoea kuwapa watu mikono kwa shangwe na furaha kama Uafrika lakini sasa hali siyo hivyo. Sasa tunasalimiana kwa ishara na yote haya ni katika juhudi za kuangamiza janga hili,” akasema.

Aidha afisa huyo wa mauzo alisema kwamba uoga wa kupata virusi hivyo umewafanya wengi kukosa kuaminiana hata wanapokuwa karibu.

“Kuna uoga mwingi sana wa kupata virusi hivi kiasi kwamba hakuna kuaminiana tena hata ndani ya familia. Nikifika ofisini mambo ni yale yale hivi kwamba watu waogopana ingawa kazi yetu lazima iendelee lakini sasa ni katika mazingira magumu ambayo hatujawahi kuyaona,” akasema Bw Ongeri.

Na kwa mwakilishi wa wadi ya Kabazi, kaunti ya Nakuru Bw Peter Mbae, hofu ya kuambukizwa virusi hivyo imemfanya kufanya kazi akitumia simu yake ya mkononi.

“Tatizo kubwa la hofu ya Corona ni kuwa siwezi kufanya kazi zangu vyema. Kwa mfano ninalazimika sasa kufanya kazi kupitia kwa rununu. Zamani pia nilikuwa nikijumuika na wananchi katika mikutano kama minne au mitano kwa siku lakini sasa hilo haliwezekani,” akasema mwakilishi huyo.

Sasa Dkt Mbae anakiri kwamba janga la Corona limebadlisha maisha yake kwa kiwango kikubwa sana.

“Mara nyingi nilikuwa nikijumuika na wananchi katika mazishi, kuongea nao katika mazingira ya kawaida lakini jambo hilo sasa hakuna tena. Ni msukumo mkuu wa mabadliko ambao lazima hata hivyo tupambane nao,” akasema Dkt Mbae.