• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Mbunge atoa Sh5 milioni na mitungi 200 ya maji kukabiliana na Covid-19

Mbunge atoa Sh5 milioni na mitungi 200 ya maji kukabiliana na Covid-19

Na LAWRENCE ONGARO

WANANCHI mjini Thika wanaendelea kuhamasishwa umuhimu wa kunawa mikono ili kuepukana na Covid-19.

Naye Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina ametoa mchango binafsi wa Sh5 milioni ili kusaidia kukabiliana na janga la Covid-19.

Alisema baada ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuamua kukatwa mishahara yao kwa asilimia 80 yeye pia kama kiongozi amejitokeza wazi kusimama na wananchi.

“Kutoa msaada ni kutoka kwa moyo na kwa hivyo ni muhimu kwangu pia kukabiliana na janga hilo kwa njia ya kifedha,” alisema Bw Wainaina.

Licha ya kufanya hayo ameamua Ambulansi ya Jungle Foundation na magari mengine mawili yawe yakizunguka katika mji wa Thika na vitongoji vyake ili kuhamasisha wananchi kuhusu janga la Covid-19.

Alipendekeza serikali itenge takribani Sh100 bilioni ambazo zinaweza kusaidia wananchi kwa miezi mitatu hivi kwa mahitaji ya chakula.

“Fedha hizo angalau zinaweza kukimu wananchi kununua chakula huku wakiwa wamejibana kwao nyumbani. Hilo ni jambo likipangwa kwa uwazi litawezekana,” alisema Bw Wainaina.

Aliitaka nchi ya China ambayo kutoka kwayo Kenya inanunua karibu asilimia 75 ya bidhaa ijaribu pia kusaidia ili kupunguzia raia mzigo wa maisha.

“Iwapo Wachina watafanya hivyo, bila shaka hata serikali itakuwa na nafasi nzuri ya kukabiliana na Covid-19,” alisema kiongozi huyo.

Alitaka serikali itafute mikakati jinsi ya kuwasaidia watoto wa mitaani ambao hawana makao.

Mbunge wa Thika Patrick Jungle Wainaina ametoa Sh5 milioni na mitungi 200 ya maji kukabiliana na Covid-19. Picha/ Lawrence Ongaro

“Watoto hao watapata shida kubwa hasa wakati huu ambapo serikali imeweka kafyu ya lazima ya kutotoka nje usiku,” alisema Bw Wainaina.

Kuhusu nguo za mitumba, alisema serikali inastahili kufufua viwanda vya nguo hasa mjini Thika ambapo karibu viwanda vitano vilifungwa miaka mingi iliyopita.

“Sisi kama nchi tunastahili tujitegemee kiviwanda na tuunde nguo bora ambazo mwananchi wa kawaida ataweza kununua kwa bei nafuu. Tukifanya hivyo tutakuwa tumepiga hatua kubwa,” alisema Bw Wainaina.

Wakati huo pia mbunge huyo alitoa mitungi 200 za maji ambazo zitatumika katika vituo tofauti kwa kunawa mikono.

Alisema baadhi ya maeneo yatakayopata mitungi hiyo ni katika vituo vya magari, vituo vya bodaboda, hospitali, sokoni, na katikati ya mji wa Thika.

Wakati wa uzinduzi huo wananchi walihamasishwa jinsi ya kunawa mikono na kuhakikisha hakuna kusalimia mwengine ovyo bila kuzingatia historia yake.

Aliwahimiza wananchi wasikubali kutembea kwa marafiki bali watulie nyumbani.

Ili kuthibitisha uzito wa hali hiyo alisema ripoti kamili inaeleza ya kwamba watu laki tano (500,000) tayari wameambukizwa na Covid-19, huku 22,000 wakifariki kutokana na homa hiyo hatari.

Aliwahimiza wananchi wafuate kanuni iliyowekwa na serikali ya kubaki nyumbani kutoka saa moja za jioni hadi 11 za alfajiri.

 

  • Tags

You can share this post!

Boris Johnson agundulika ana virusi vya corona

‘Shujaa na Lionesses pamoja na KRU hazitafaidika na...

adminleo