• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
Mvua yatatiza shughuli za uchukuzi mitaa kadhaa Nairobi

Mvua yatatiza shughuli za uchukuzi mitaa kadhaa Nairobi

Na SAMMY WAWERU

MVUA nyingi ilishuhudiwa Alhamisi jioni katika baadhi ya mitaa katika Kaunti ya Nairobi na kusitisha kwa muda shughuli za usafiri na uchukuzi.

Hali hiyo pia ilisababisha kupotea kwa nguvu za umeme kwa saa kadhaa.

Mitaa iliyoathirika ni pamoja na Kahawa Wendani, Githurai, Kahawa West, Zimmerman, Mwiki na Kasarani.

Mvua hiyo iliyoanza mwendo wa saa kumi na moja za jioni, iliendelea kwa zaidi ya saa tatu mfululizo. Matatu zililazimika kuegeshwa kwa muda ili kuruhusu mvua hiyo ya mafuriko kupungua.

Licha ya hali hiyo, wahudumu wa matatu walitumia fursa hiyo kuvuna pesa kwa kupandisha ada ya nauli mara dufu.

Kwa mfano, matatu yanayohudumu kati ya Githurai – Roysambu, yalitoza nauli ya Sh40, kutoka Sh20 au Sh10 ada ya kawaida.

Wanabodaboda nao, hususan wenye mwavuli walifuata nyayo za wahudumu wa matatu kuongeza nauli, sawa na wa tuktuk.

“Kutoka jijini Nairobi hadi Roysambu nimelipa nauli ya Sh150, ada ya kawaida huwa Sh50. Ninashangaa iwapo bei ya mafuta huongezeka mvua inaponyesha,” akalalamika Peris Wafula, mkazi.

Uongezaji nauli miongoni mwa wahudumu wa matatu ni tabia inayoshuhudiwa mara kwa mara nchini, hasa wakati wa majanga. Huku taifa likiendelea kujawa na taharuki kufuatia mkurupuko wa Covid-19, baadhi ya matatu zimeongeza nauli kupita kiasi haswa kwa wanaosafiri kuelekea mashambani kutoka mijini.

You can share this post!

‘Shujaa na Lionesses pamoja na KRU hazitafaidika na...

Corona yaendelea kushika wakubwa

adminleo