Makala

TAHARIRI: Wanaspoti wakae fiti katika janga hili

March 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

KUTOKANA na tishio baya la virusi vya corona, shughuli zote duniani ikiwemo michezo zimesimama.

Hii inamaanisha kuwa pana upungufu wa fursa za kufanya mazoezi yanayoweza kuwaweka fiti wachezaji huku wakisubiri kuisha kwa virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

Kilicho dhahiri ni kwamba ni timu zilizojiweka tayari pekee ambazo zitakang’ara katika mashindano mbalimbali kama vile ligi kuu na kabumbu ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mchezo wa timu nyingi utakuwa umedorora kutokana na wachezaji kutofanya mazoezi ya kutosha wakati huu.

Hivyo basi, jinsi wataalamu wa michezo walivyonasihi, ni aula wanasoka hawa kuendelea na mazoezi ya kutosha ndipo wakati wa kurejelewa kwa mashindano hayo, wasijipate wakifanya kazi ovyo viwanjani.

Waama, inafahamika kuwa baadhi ya wanamichezo waliokuwa wamejiandaa kwa mashindano mbalimbali ya kimataifa ya mwaka huu hasa Michezo ya Olimpiki, wamevunjika mioyo baada ya michezo hiyo kuahirishwa hadi mwaka ujao.

Kwa mfano, mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge, akionekana kusema kwa niaba ya chipukizi waliokuwa wamefuzu kushiriki Olimpiki za mwaka 2020 zilizopangiwa kufanyika jijini Tokyo, Japan, alisema kuwa wengi walivunjika moyo maadamu hawajui kama watakuwa katika kiwango kizuri cha ushindani mwaka ujao michezo hiyo itakapofanyika.

Hii inamaanisha kuwa walikuwa wamejiandaa vya kutosha kung’ara ila kutokana na kusongeshwa kwa mashindano hayo hadi mwaka ujao, huenda maandalizi yao yakawa yamedidimia na hivyo basi kushusha uwezo wao wa kushindana na hata kutwaa medali.

Hata hivyo, tunawatia shime kuwa, maadamu hili ni tatizo la ulimwengu mzima, anayelenga kufana mwakani atalazimika kuendelea na mazoezi ya kila mara, hususan baada ya kutokomezwa kwa corona.

Hiyo ndiyo motisha waliyo nayo wanavoliboli wa Malkia Strikers ambao watawakilisha bara hili katika Michezo hiyo ya Olimpiki.

Kwao, wanasadiki kuwa kusongeshwa kwa mashindano hayo kutawasaidia hata kujiweka vyema zaidi.

Kimsingi tunacholenga kuwahimiza wanamichezo wetu ni kuwa waangalie jinsi ya kutumia janga hili kwa manufaa yao wenyewe badala ya kutishika kutokana na mvurugiko huu.