• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
CORONA: Visa vyafika 42, wanaoeneza uvumi mitandaoni waonywa

CORONA: Visa vyafika 42, wanaoeneza uvumi mitandaoni waonywa

NA FAUSTINE NGILA

Idadi ya watu walio na virusi vya corona imeongezeka Jumapili na kufika 42 baada ya watu wengine wanne kuthibitishwa kuugua ugonjwa huo.

Akihutubia Wakenya Jumapili, Waziri wa afya Mutahi Kagwe alisema kati ya wanne hao, mmoja ni Mkenya na wengine watatu ni raia wa Amerika, Cameroon na Burnika Faso.

Alisema watatu kati ya wanne hao wako jijini Nairobi na mmoja Mombasa. Kati ya hao 42 , 24 ni wanaumme na 18 ni wanawake.

Kaunti ya Nairobi inaongoza na kesi 31 ikifuatwa na Kilifi yenye visa 6, Mombasa vitatu, Kwale na Kajiado kimoja.

Wakati huo huo, waziri huyo aliwaonya vikali viongozi wanaochapisha jumbe za kupotosha umma kwenye mitamdao ya kimajii. “Watachukuliwa hatua, hatuwezi kukubali wanasiasa kupotosha wananchi,” alisema.

Jumamosi, Mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie alichapisha ujumbe mrefu mtandaoni Facebook akidai kuwa Kenya kwa sasa ina watu 7,000 waliotengwa, madai ambayo serikali imepinga vikali.

Jumapili jioni, mbunge huyo aliandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Kabete.

Bw Kagwe alisema kuwa watu waliotengwa kufikia sasa ni 2050, na kuwa wengine 1426 wanafuatiliwa huku 15 wakiwa wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kukamilisha muda wa kutengwa wa siku 14.

Ili kudhibiti ugonjwa huu, alisema kupimwa kwa watu waliofika humu nchini kuanzia Jumamosi kunaindelea.

Waziri huyo alisema kuwa watu 18 wanasubiri matokeo kutoka hospitali ya Mbagathi.

“Watakaopatikana na virusi hivyo watatengwa. Inasikitisha kuwa baadhi ya viongozi wanaeneza habari za uwongo kuhusu virusi vya corona kwa mitandao ya kijamii ili wapate umaarufu wa kisiasa. Tabia hii ikome,” alionya.

Aliwarai Wakenya kuzingatia usafi wa hali ya juu na kutotangamana.

Aliwapongeza maafisa wa sekta ya kibinafsi kwa kusaidia serikali kupata vifaa vinavyoweza kutumika hospitalini na maeneo ya kuwatenga waathiriwa.

You can share this post!

CORONA: Kimya makanisani, waumini wakimbilia YouTube

Polisi wanyama waadhibiwe, kafyu ianze saa tatu – Dkt...

adminleo