Habari MsetoSiasa

Mbunge apata virusi wengine wakimulikwa

March 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DAVID MWERE

BUNGE limewasilisha majina ya wabunge na wafanyikazi wapatao 50 kwa Wizara ya Afya ili watafutwe na wachunguzwe kimatibabu kwani inahofiwa huenda wameambukizwa virusi vya corona.

Hii ni baada ya kufichuka kuwa kuna uwezekano mkubwa wabunge hao walitangamana na Mbunge wa Rabai William Kamoti, ambaye tayari amethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Mbunge huyo anaaminika aliambukizwa alipotangamana na Naibu Gavana wa Kilifi Gideon Saburi, ambaye awali alipatikana anaugua coronavirus.

Habari zilisema wawili hao watangamana katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori mnamo Machi 9.

Jana, afisa wa bungeni ambaye aliomba asitajwe jina alisema Bw Kamoti amelazwa hospitalini.

‘Bunge limearifu Wizara ya Afya iwatafute na kuwapima watu wote ambao mbunge huyo alitangamana nao, wakiwemo wabunge wenzake na wafanyakazi wa bunge,’ afisa huyo alisema.

Rekodi zinaonyesha mbunge hiyo alikuwa bungeni Machi 17 kwa dakika 19, saa chache kabla bunge kuvunja vikao vyake hadi Aprili 14.

Mingoni mwa wale watakaohitajika kupimwa kama waliambukizwa na kutengwa ni wanachama wa kamati ya haki na sheria (JLAC) na ya mamlaka yaliyogawanywa ambapo Bw Kamoti ni mwanachama.

Inaaminika kamati hizo mbili zilizo na wanachama 38 huenda ziliandaa mikutano na mbunge huyo akahudhuria baada ya kukutana na Bw Saburi.

Wafanyakazi wa bungeni ambao huhudumia kamati hizo mbili pia watatakikana kuchunguzwa kimatibabu.

Mbali na wanachama wa kamati hizo mbili, wizara pia inatafuta wabunge ambao huenda walitangamana na Bw Kamoti wakati alipokuwa ndani ya bunge mnamo Machi 17.

Wataalamu wa afya wanasema inachukua siku 14 kabla mtu aliyeambukizwa virusi vya corona kuanza kuonyesha dalili za maambukizi.

Dalili hizo zinajumuisha kukohoa, joto jingi mwilini, kutokwa kamasi na udhaifu wa viungo vya mwili.

Bw Saburi kwa sasa anaendelea kupokea matibabu alivyoambukizwa akiwa ziarani Ujerumani mapema mwezi huu.

Wizara ya Afya imethibitisha ilitambua kulikuwa na watu 122 waliotangamana naye kwa karibu.Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alitangaza pia kwamba Bw Saburi atashtakiwa mahakamani punde atakapopona, kwa kukiuka agizo la serikali lililotaka walioingia nchini kutoka ng’ambo wajitenge kwa siku 14.

Ujerumani ni mojawapo ya mataifa ya Ulaya ambayo yameathiriwa sana na ueneaji wa virusi vya corona, huku Amerika ikipita Uchina kwa idadi ya maambukizi.

Kufikia jana jioni, watu zaidi ya elfu 868 kutoka mataifa 199 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo vilivyoanza nchini China mwishoni mwa mwaka jana, huku wengine zaidi ya elfu 32 wakifariki.

Amerika ilikuwa ingali ikiongoza katika maambukizi kufikia jana ikiwa na visa elfu 125 na kufuatwa na Italia yenye wagonjwa elfu 92.