CORONA: Daktari motoni kwa kukataa kuhudumia wagonjwa
NA RUTH MBULA NA FAUSTINE NGILA
DAKTARI mmoja katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) yuko taabani na huenda atapigwa kalamu baada ya kudinda kuwahudumia wagonjwa, akitaja ukosefu wa maandalizi kutokana na virusi vya corona.
Hospitali hiyo ambayo ndiyo kubwa zaidi katika eneo la Nyanza Kusini, sasa inapanga kumchukulia hatua za kinidhamu ambazo zinalenga kumtimuakazini daktari huyo.
Katika barua iliyoonekana na Taifa Leo Dijitali, afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo Emock Ondari alisema kitendo cha daktari huyo kilionyesha utovu wa nidhamu ya kitaaluma, na anafaa kuadhibiwa.
“Wanakuwakilisha, iwapo wapo, wanafaa kufika katika ofisi hii kabla ya saa 72 kutoka siku ya kuandikwa kwa barua hii, ukikosa basi hatua iliyopangwa itachukuliwa dhidi yako bila hata kushirikishwa,” barua hiyo ilisema.
“Ulidai hakuna barakoa za N95 licha ya kupewa barakoa za upasuaji, maji na sabuni.”