Habari Mseto

Viduka vya vinyozi na saluni vyafungwa

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

IDARA ya Afya ya Umma, Kaunti ya Lamu, imesimamisha huduma zinazotolewa na saluni na vinyozi zaidi ya 200 katika harakati za kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona eneo hilo na nchini kwa jumla.

Afisa wa Idara ya Afya ya Umma, Kaunti ya Lamu, Ahmed Muhsin, alisema waliafikia hatua hiyo ya kuzifunga saluni na vinyozi kwa muda kote Lamu kwani ni vigumu wa wahudumu wa biashara hizo kuzingatia matakwa ya kudhibiti umbali wa mita moja na usafi unaohitajika kwa jumla ili kuepuka kuambukizwa Covid-19.

Bw Muhsin alishikilia kuwa kuanzia juma hili kuendelea ni marufuku kwa saluni na wahudumu wa vinyozi kuendeleza shughuli zao na kwamba yeyote atakayepatikana akikaidi amri hiyo atakamatwa na kushtakiwa na hata kupokonywa leseni yake ya kufanyia kazi.

Biashara ya saluni na vinyozi kaunti ya Lamu imenoga zaidi kwenye miji ya Lamu, Mpeketoni, Hindi, Mokowe na Witu.

Afisa huyo wa Idara ya Afya ya Umma aliwataka wananchi kuzingatia masharti na maelekezo yote yanayotolewa na serikali kila kuchao ili kuzuia kusambaa kwa virusi hatari vya Corona nchini.

“Tumeafikia kuzifunga saluni na vinyozi vote kwa muda kote Lamu kama njia mojawapo ya kukabiliana na kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona. Tumefunga zaidi ya saluni na vinyozi 200 kufikia sasa. Biashara hizo ni hatari kwani ni rahisi kuchangia maambukizi kutokana na kwamba mhudumu na mhudumiwa lazima wakaribiane. Tutazifungua tu punde hali itakapodhibitiwa nchini,” akasema Bw Muhsin.

Kufuatia amri hiyo, wahudumu wa vinyozi na saluni mjini Lamu wameeleza wasiwasi wao kwamba huenda wakafungiwa nyumba zao kutokana na ukosefu wa fedha za kulipia kodi nyumba hizo.

Mmiliki wa LAPSSET Kinyozi, Bw Lincon Matu, alisema kusimamishwa kwa biashara hizo ni pigo kubwa kwao.

“Sisi hatuna njia nyingine ya kujipatia riziki ya kila siku isipokuwa hizi huduma za vinyozi. Wametufungia biashara ghafla. Tuko na wasiwasi kwani huenda wengine wetu tukafungiwa nyumba kwa kukosa kodi, Serikali itusaidie hata kama ni kutupa mikopo maalum wakati huu wa janga la virusi vya Corona ili kujimudu,” akasema Bw Matu.

Naye Bi Margaret Waithera ambaye ni mhudumu wa saluni moja kisiwani Lamu aliikashifu serikali ya kaunti hiyo kwa kukosa kuwafahamisha mapema kuhusiana na mpango wao wa kufunga biashara za vinyozi na saluni.

Bi Waithera aliiomba serikali ya kaunti kuwapa angalau muda wa wiki moja kujipanga kabla ya kushurutishwa kufunga biashara hizo.

“Wametuamuru kufunga biashara zetu ghafla bila ya kutupa notisi ya mapema ili kujipanga. Tutakula nini kama leo hii tunaambiwa tuzifunge biashara zetu? Tunaomba kaunti ituonee imani kwa kutuongezea wiki moja zaidi kabla ya kuamuru biashara zetu zifungwe kwa sababu ya Corona,” akasema Bi Waithera.